Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima ameungana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na watanzania wwote kwa jumla kutoa pole kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki kwa kuondokewa na aliyekuwa Waziri Mkuu Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Edward Ngoyai Lowassa.
Mhe. Malima ametoa Salamu hizo za pole Februari 12, 2024 wakati akifanya mahojiano na Mwandishi wa habari hizi Ofisini kwake.
Mkuu huyo wa Mkoa amesema Mhe. Edward Lowassa atakumbukwa katika historia ya Tanzania kwa kusimamia ujenzi wa shule za Kata hapa nchini ambazo zimewasaidia wananchi wa kipato cha chini kupata fursa ya elimu huku akibainisha kuwa jambo hilo liliifanya Tanzania kuwa kinara wa elimu Afrika Mashariki na Kati.
"...jambo lingine ambalo historia itakumbukwa siku zote ni kwamba wakati Mhe. Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete wakati huo alipotangaza nia ya kuwa na shule za sekondari kwenye kila kata msimamizi wa zoezi lile alikuwa Waziri Mkuu Mhe. Edward Lowassa..." amesema Mkuu wa Mkoa.
Aidha, Mhe. Malima amesema Hayati Edward Lowassa alikuwa shujaa hasa pale alipochukua hatua ya kujihuzuru katika nafasi yake ya Waziri Mkuu. Ameongeza kuwa Mhe. Lowassa alionesha ukomavu wa kisiasa na nia yake ya kuwatumikia wananchi hususan alipogombea nafasi ya Urais kupitia chama pinzani.
MWISHO.
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.