Imeelezwa kuwa, mara baada ya maadhimisho ya miaka sitini ya uhuru, mwelekeo wa Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ni kuelekeza nguvu zote katika kufanya kazi na kuwanyang’anya maeneo wale wote waliojilimbikizia maeneo bila kuyaendeleza na kuwapatia watu wenye uhitaji kwa ajili ya kuzalisha zaidi.
Hayo yameelezwa Disemba 8 mwaka huu na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine shigela wakati wa maadhimisho ya miaka 60 ya uhuru yaliyofanyika kimkoa katika uwanja wa CCM Tangani katika Mji Mdogo wa Ifakara Wilayani Kilombero Mkoani humo.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela (mwenye shati la Kitenge) akitembelea moja ya mabanda siku ya maadhimisho ya miaka 60 ya uhuru. Hili ni banda la kiwanda cha kusindika asali
Amesema, miaka 61 ya uhuru tunayoanza nayo sasa ni muda wa kuendelea kuwatumikia wananchi kwa unyenyekevu huku akiwataka viongozi ambao bado wana dhana potofu ya wao kufanya kazi kama watawala wa kikoloni kubadilika na kufuata mwelekeo wa Serikali wa kuwatumikia wananchi kwa kusikiliza kero zao na kutatua changamoto zinazowakabili.
“wale watu wenye kujilimbikizia maeneo bila kuyaendeleza miaka 61 tunayoanza nayo tutafuata sheria kuwanyang’anya ili tuwagawie watu wenye uhitaji ili waendelee kuzalisha kwenye mashamba” amesema Martine Shigela.
“wale baadhi ya watawala na viongozi na watumishi wanaodhani wataendelea kuishi kama mabwenyenye kama wakoloni lazima waendelee kuwawaunyenyekevu katika kuwatumikia wananchi” ameongeza na kusisitiza.
Mkuu wa Mkoa na Katibu wa CCM Mkoa wa Morogoro wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Wakuu wa Wilaya za Mkoa huo
Akifafanua zaidi juu ya mafanikio yaliyopatikana kwa kipindi cha miaka 60 ya uhuru Mkoani humo hususan katika sekta ya Elimu amesema, idadi ya shule na vyuo imeongezeka kwa kiasi kikubwa na kubainisha kuwa Shule za Msingi mwaka 1961 zilikuwa 12 kwa sasa zipo shule 963, shule za sekondari mwaka 1961 zilikuwa 08 kwa sasa zipo shule 246.
Wabunge wa Viti Maalum wakiwa katika picha ya pamoja na Mhe. RC. kushoto ni Mhe. Christine Ishengoma
Kwa upande wa Vyuo vya kati amesema mwaka 1961 kulikuwa na vyuo 03 kwa sasa Mkoa huo una vyuo 62 na vyuo vikuu amesema mwaka 1961 hakukuwa na chuo Kikuu chochote lakini sasa Mkoa wa Morogoro peke yake una vyuo vikuu vitano.
Wenyeviti wa Halmashauri za Mkoa wa Morogoro wakiwa katika picha ya pamoja na Mkuu wa Mkoa siku ya maadhimisho ya mika 60 ya Uhuru kimkoa. wa nne kushoto ni Meya wa Manispaa ya Morogoro Mhe. Pascal Kihanga na watatu kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Kilombero Hanji Godigodi
Kuhusu Afya, Mkuu huyo wa Mkoa amesema Mkoa ulikuwa na upungufu wa Hospitali, vituo avya pamoja na zahanati, lakini hadi tunapoadhimisha miaka 60 ya uhuru Mkoa unajivunia kuwa na hospitali 18, vituo vya Afya 57 na zahanati zisizopungua 387 ndani ya Mkoa wa Morogoro peke yake.
Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Kilombero
Jeshi la akiba Kilombero likiwa katika picha ya pamoja na Mkuu wa Mkoa
Kwa upande wa viwanda Martine Shigela amesema tunapoadhimisha miaka sitini ya Uhuru Mkoa ulikuwa na viwanda vichache na vyenye uzarishaji mdogo, kwa sasa ndani ya Mkoa wa Morogoro viwanda vimeongezeka na vikiwemo viwanda vya nguo, kuchakata mchele, viwanda vya magunia na viwanda vya kuzarisha Sukari vya Mtibwa na Kilombero ambavyo viko kwenye ya kuongeza uzarishaji.
Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri Mkoa wa Morogoro
Makatibu Tawala wa Wilaya za Mkoa huo nao walishiriki maadhimisho hayo
Akitolea mfano wa kiwanda cha Sukari cha Kilombero ambacho kilijengwa mwaka 1961 miaka sitini iliyopita Shigela amesema kiwanda hicho kimeanza kazi ya ujenzi wa kiwanda kingine ili kuongeza uzalishaji wake ujenzi utakaoghalimu shilingi Bilioni 575 Serikali ikiwa inachangia asilimia 25 ya gharama hiyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi Joanfaith Kataraia (kushoto) akipokea box la chaki zilizotengenezwa na moja ya viwanda vidogo vya Ifakara kinachojulikana kwa jina la Ifakara Standard Chalk mara baada ya Mhe. RC kukitembelea wakati anatembelea mabanda ya maonesho wakati wa Maadhimisho ya miaka 60 ya uhuru
Katibu Tawala Msaidizi upande wa Utawala na Rasilimali watu Ndg. Herman Tesha (mwenye suti nyeusi) akipokea box la chaki kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Bi. Mariam Mtunguja
Amesema kiwanda hicho kwa sasa kinasindika miwa tani 100 kwa saa ambapo kiwanda kinachojengwa sasa kitakuwa na uwezo wa kusindika tano 407 za miwa kwa saa, ni Zaidi ya mara 4 ya uzalishaji wa awali hivyo amesema yapo mategemeo ya kuondokana na upungufu wa Sukari hapa nchini lakini pia kiwanda hicho kinakwenda kukidhi hitaji la wakulima wa Miwa ambao wameongezeka na kuongeza uzalishaji wao wa miwa iliyokuwa inakosa mahali pa kusindika.
picha ya pamoja na RC na vongozi wa Chama Tawala wa ngazi mbalimbali Mkoani Morogoro
Wazee Maarufu wa Mji mdogo wa Ifakara wakiwa katika picha ya pamoja na Mkuu wa Mkoa mara baada ya maadhimisho hayo
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kilombero Hanji Godigodi pamoja na kueleza mafanikio yaliyopatikana ndani ya maadhimisho ya miaka 60 ya uhuru, ameishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa kupeleka Wilayani humo fedha za UVIKO - 19 Tsh. 2.880 Bil. kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa 140 pamoja na bweni moja la shule maalum.
mwanafunzi Laitnes Kambi wa shule ya msingi Tundu Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro, akijiandaa kupokea zawadi ya Tsh. 500,000/= ya uandishi bora wa Insha kwa shule za Msingi Mkoani Morogoro.aliibuka mshindi wa kwanza wa mashindano hayo.
washindi wengine wa mashindano hayo wakipewa zawadi zao, huyu ni kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.
Hata hivyo Mkuu huyo wa Wilaya amewapongeza wananchi wa Wilaya hiyo kwa kushiriki katika ujenzi wa miradi ya maendeleo kwani kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita wananchi hao wamechangia nguvu kazi zao zenye thamani ya Tsh. 3.51 Bil hivyo pamoja na kuwapongeza ametoa wito kwao kuendeleza utamaduni huo ni suala msingi kwao na kwa vizazi vijavyo.
Wananchi wakifurahia maadhimisho ya miaka 60 ya uhuru, furaha yao iliongezeka walipopongezwa na DC wao kwa ushirikiano wao wa kuchangia nguvu kazi kwenye masuala ya maendeleo. hapo wakiongozwa na msanii mmojawapo kutoka Ifakara
Kwa upande wake Mbunge wa viti Maalum Mhe. Christine Ishengoma akitoa salamu zake kwa niaba ya wabunge wote wa Mkoa wa Morogoro yeye amemkumbuka Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kuwa ameifanyia mambo makubwa nchi hii na ndiye mwanzilishi wa uwepo wa Amani na Utulivu ndani ya nchi hii jambo ambalo ni tunu kubwa ya kuienzi kwa muda wote hata tunapoadhimisha miaka hii 60 ya uhuru.
Maadhimisho hayo ya miaka 60 ya uhuru ambayo kimkoa yamefanyika Disemba 8 Ifakara yalikuwa na kaulimbiu “Tanzania Imara Kazi iendelee”.
Wauguzi na madaktari wa Hospitali ya St.Francis Ifakara wakiwa katika maandamano wakati wa Maadhimisho ya miaka 60 ya uhuru yaliyofanyika kimkoa Disemba 8 mwaka huu Ifakara
Hawa ndio walioinogesha sherehe hiyo ya maadhimisho ya miaka 60 ya Uhuru, walivitawala visemeo vyao kisawasawa na kufaulu kusherehesha wananchi vilivyo. hawa (ma MCs) wako vizuri. hongereni kwenu ma MC wetu.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.