Bwana Vicent kayombo Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais - TAMISEMI akizungumza na Maafisa wa elimu wa Mikoa na Halmashauri nchini kwenye ufunguzi wa Mafunzo endelevu ya Walimu Kazini.
Maafisa elimu wa mikoa na Halmashauri hapa nchini wametakiwa kusimamia kwa usahihi fedha za miradi ya maendeleo hususan fedha zinazoendelezwa kwenye ujenzi wa miundombinu ya shule yakiwemo madarasa kwa kuzingatia miongozo itakayotolewa na Serikali.
Agizo hilo limetolewa Januari 27, mwaka huu na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa - TAMISEMI Prof. Riziki Shemdoe kupitia hotuba yake iliyosomwa na Bwana Vicent Kayombo ambaye ni Kaimu Katibu Mkuu wa TAMISEMI kwenye ufunguzi wa kikao cha usimamizi wa mafunzo endelevu ya walimu kazini (MEWAKA) kwa viongozi na waratibu wa MEWAKA ngazi za mikoa na Halmashauri, uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa chuo cha Uwalimu Mkoani Morogoro.
Akifafanua zaidi Bwana Vicent Kayombo amesema Muda si mrefu fedha za utekelezaji wa mradi wa BOOST zitatumwa Mikoani, Halmashauri, na shuleni ikiwemo fedha za ujenzi wa miundombinu ya shule hivyo wanatakiwa kuzisimamia fedha hizo kwa usahihi na kukamilisha miradi yote ya ujenzi kwa wakati na kwa kuzingatia miongozo itakayotolewa na Serikali.
Aidha, Kayombo ameongeza kuwa zaidi ya Shilingi Bilioni 230 zitatumwa moja kwa moja shuleni, kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa, na Sekretarieti za Mikoa kwa ajili ya utekelezaji wa Miradi hiyo.
"...Ni marufuku kutumia fedha au kutekeleza shughuli yoyote kinyume na miongozo ya miradi itakayotolewa". Kaimu Katibu huyo.
Sambamba na hilo, Bw. Kayombo kwa niaba ya Katibu Mkuu TAMISEMI amewaagiza Maafisa elimu hao Kuimarisha usalama wa wanafunzi kwa kushirikiana na jamii pamoja na viongozi wa Serikali za Mitaa kutokana na kuongezeka kwa vitendo vya ukatili na unyanyasaji dhidi ya watoto.
Pamoja na hayo ameongeza kuwa iwekwe mifumo itakayowawezesha kuzuia na kubaini kama vitendo hivyo vinafanyika shuleni na kuchukua hatua stahiki kwa mujibu wa sheria na miongozo iliyopo.
Kwa upande wake Mratibu wa Mradi wa BOOST Bw. Ally Swalehe amesema mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa sera ya elimu na mafunzo ya mwaka 2014, mafunzo hayo yanahusisha jumla ya washiriki 286, wakiwemo maafisa elimu wa mikoa yote 26, maafisa elimu wa elimu ya awali na msingi kutoka Halmashauri 52, Wadhibiti ubora wa shule kutoka Halmashauri 52 na Waratibu wa Mafunzo endelevu ya walimu kazini kutoka halmashauri 52.
Nae Afisa Elimu Mkoa wa Morogoro Bi. Germana Mung’aho akitoa salam za Mkoa na kuwakaribisha wageni ndani ya Mkoa huo amesema wapo tayari kuyapokea mafunzo hayo na kwenda kuyafanyia kazi kwa manufaa ya walimu waliopo shuleni ili kuongeza ufanisi katika kazi zao.
Lengo kuu la MEWAKA ni kuimarisha utendaji wa walimu kwa kuwawezesha kukua kitaaluma ili kuboresha matokeo ya ufundishaji.
Aidha, imeelezwa kuwa mafunzo hayo ni muhimu kwa sababu yatawawezesha walimu kupata mbinu mpya za kufundishia na kujifunzia, yataongeza motisha ya walimu kufanya kazi kwa kuwa watapata usaidizi wa kitaalamu kutoka kwa walimu wenzao, kuweka malengo yao ya kitaaluma yanayofikika, na kupata maarifa mbalimbali kuhusu masomo wanayofundisha.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.