Maafisa Manunuzi Mkoa wa Morogoro wametakiwa kuzingatia sheria, Kanuni na taratibu za Manunuzi ya Umma ili kuepusha Halmashauri zao kuendelea kupokea kazi, vifaa na huduma ambazo ziko chini ya kiwango.
Maagizo hayo yametolewa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Mhandisi Emmanuel Kalobelo Novemba 11 mwaka huu wakati akifungua kikao kazi cha siku tano cha Maafisa Manunuzi kutoka Mamlaka za Serikali za Mitaa Mkoani humo kinachoendelea VETA katika mji mdogo wa Mikumi.
Baadhi ya Maafisa Manunuzi walioshiriki kikao hicho
Mhandisi Kalobelo amesema hali hiyo ya kupokea kazi, vifaa na huduma ambazo ziko chini ya kiwango kinatokana na Wakuu hao wa Manunuzi kutozingatia taratibu na miongozo iliyopo ikiwa ni pamoja na kutoteua ipasavyo Kamati za Ukaguzi wa kazi au vifaa vinavyonunuliwa na Halmashauri zao.“hamteui ipasavyo Kamati za Ukaguzi wa kazi au vifaa vinavyonunuliwa na Halmashauri zenu kwa kuzingatia miongozo. hamfanyi hiyo kazi kikamilifu”. Alisema Mhandisi Kalobelo.
“Nendeni mhakikishe sheria, kanuni, taratibu na miongozo ya manunuzi ya Umma inazingatiwa yote bila kukwepesha” alisisitiza na kuagiza Mhandisi huyo.
Aidha, Mhandisi Kalobelo amewataka Maafisa Manunuzi katika kikao hicho kuhakikisha wanapata ufumbuzi wa changamoto zote za kutotumia mfumo wa Manunuzi kwa njia ya Kielektroniki (Tanzania National e – Procurement System – TANePS).
Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Mhandisi Emmanuel Kalobelo (aliyesimama) wakati akifungua kikao kazi cha Maafisa Manunuzi
Akifafanua zaidi, Mhandisi Kalobelo amesema Serikali kupitia kwa Katibu Mkuu ambaye pia ndiye Mlipaji Mkuu wa Serikali (Wizara ya Fedha na Uchumi) iliekeza Taasisi zote za Umma kutumia Mfumo wa TANePS kuanzia mwezi Januari Mwaka huu,Hivyo Muhandisi Kalobelo amesema hatarajii baada ya kikao hicho kuona Halmashauri ambayo haitumii mfumo huo katika kufanya manunuzi yake.
Baadhi ya washiriki wakisikiliza kwa makini hotuba ya mgeni rasmi
Aidha, Maafisa hao Wametakiwa kuachana na tabia ya kuchelewesha manunuzi ya kazi au huduma mbalimbali za Serikali yanayofanyika katika Halmashauri wanazofanyia kazi kwa sababu imeonekana sababu za ucheleweshaji huo mara nyingi unatokana na Idara zao.
Katika hatua nyingine Mhandisi Kalobelo amewataka Wakuu wa Vitengo hivyo vya Manunuzi kuboresha mahusiano baina yao na Idara nunuzi ndani ya Halmashauri badala ya hali ya sasa ambayo wanatuhumiwa kuwa na mahusiano mazuri zaidi na Wakandarasi kuliko Idara nunuzi hivyo kupunguza ufanisi wa kazi za Umma zinazolenga kuwanufaisha watanzania.
Kwa upande wake Kaimu Katibu Tawala Msaidizi anayesimamia Serikali za Mitaa Leopold Ngirwa amesema lengo la kikao kazi hicho ni kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazokwamisha baadhi ya Halmashauri kutotekeleza agizo la Serikali la kutumia mfumo wa TANePS, huku akiwakumbusha Wakurugenzi wa Halmashauri zote Mkoani humo kutoa mazingira wezeshi kwa Maafisa Manunuzi wao kuhakikisha wanautumia mfumo huo kwa manufaa na ustawi wa wananchi.
Kaimu Katibu Tawala Msaidizi anayeshughulikia Serikali za Mitaa Leopold Ngirwa akifuatilia hotuba ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro
Naye Mshauri wa Mradi wa maboresho ya Usimamizi wa Fedha za Umma (PFMRP) Mkoa wa Pwani na Morogoro Bi. Donatila Kileo amewashauri washiriki waliohudhuria mafunzo hayo kuzingatia yote wanayofundishwa katika kikao hicho maana serikali inataka wafanye manunuzi kupitia huo mfumo na si vinginevyo.
Kwa niaba ya washiriki wa kikao hicho Bi. Salima Rajabu ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Manunuzi kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Gairo amewataka washiriki wenzake kubadilika na kutekeleza majukumu yao kwa juhudi na maarifa kama walivyoagizwa na mgeni rasmi.
Hadi Juni mwaka huu, baadhi ya Taasisi zilikuwa hazijaanza kuutumia mfumo huo huku ukosefu wa Uadilifu kwa baadhi ya wataalamu wa idara za Manunuzi Serikalini ikitajwa kuwa ni sababu kuu ya kutoutumia mfumo wa TANePS na kuwa dalili kwa baadhi ya Maafisa Manunuzi kunufaika na mfumo uliokuwa unatumika zamani na hivyo kuhofu mfumo wa TANePS kuwakosesha fursa hiyo.
Utekelezaji wa mfumo huo ni kwa mujibu wa sheria ya manunuzi ya Umma ya mwaka 2011 na kanuni zake za mwaka 2013 zinazotaka shughuli zote za manunuzi kufanyika kwa msingi wa UWAZI ili thamani ya fedha za watanzania iweze kuonekana kwenye miradi, huduma au vifaa hivyo vinavyonunuliwa.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.