Katika juhudi za kukabiliana na vifo vya kinamama wajawazito na watoto wachanga hapa nchini Serikali inaendesha mafunzo ya mfumo wa usafirishaji wa dharura kwa mama mjamzito na mtoto yaani - M-mama yanayotolewa kwa wataalamu wa TEHAMA ngazi ya Mikoa na Hospitali za rufaa.
Mkurugenzi Idara ya TEHAMA Ofisi ya Rais -TAMISEMI Erick Kitali wakati akifungua mafunzo ya usafirishaji wa dharura kwa mama mjamzito na mtoto M-MAMA.
Akifungua mafunzo hayo yaliyofanyika Queen Hotel katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro Mkurugenzi Idara ya TEHAMA Ofisi ya Rais -TAMISEMI Erick Kitali amesema Pamoja na juhudi za Serikali, bado vifo vitokanavyo na uzazi vimeendelea kuwa juu.
Amesema, takwimu zinaonesha uwiano wa 578 kati ya vizazi hai 100,000 sawa na asilimia 18 ya vifo vyote vya wanawake wenye umri wa miaka 15-49.
Kitali amebainisha kuwa mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uelewa zaidi watalaam hao wa TEHAMA ili kukabiliana na changamoto za ucheleweshwaji unaosababisha matokeo mabaya ya uzazi kama vifo au ulemavu wa kudumu kwa wajawazito na watoto wachanga.
Mchambuzi wa Mifumo ya TEHEMA OR-TAMISEMI Shabani Zungiza amesema tayari Mikoa 16 imeshaanza kutumia mfumo huo wa M - Mama ambapo sasa mgonjwa anaweza kupata huduma ya kupiga simu bure kupitia namba 115 ili kupata huduma hiyo.
“Tunafahamu tuna Changamoto kubwa hususani kwenye mifumo ya TEHAMA lakini maafisa TEHAMA ambao wapo ngazi ya Mikoa, Halmashauri na Hospitali za rufaa ni miongoni mwa watu ambao wanatakiwa kuhamasisha namna ya utumiaji wa mfumo huo” ameeleza Shabani Zungiza.
Kwa upande wake Afisa TEHAMA Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Ashura Sadiki amesema awali kulikuwa na changamoto kubwa ya mawasiliano lakini kupitia mfumo huo umerahisisha upatikanaji wa haraka wa huduma hiyo kwa akinamama wajawazito.
Pichani ni baadhi ya washiriki wa mafunzo ya usafirishaji wa dharura kwa mama mjamzito na mtoto M-MAMA wakiwa kwenye mafunzo hayo.
“ Mama mjamzito pamoja na mtoto ni watu ambao huwa mabadiliko yanatokea ghafla anaweza kupungukiwa damu ghafla au mtoto anaweza kubadilika ghafla, kwa hiyo wanahitaji huduma hiyo ambayo ni ya haraka kwa hiyo Serikali imekuja na mfumo wa M-mama ambao unarahisisha mtoa huduma au anayehitaji huduma kupata huduma kwa haraka” amesema Ashura Sadiki.
Mwisho
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.