Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Loata Ole Sanare amewaagiza Maafisa Ugani Mkoani humo kutumia muda wao mwingi kuwafundisha wakulima kwa vitendo namna bora ya kulima zao la mahindi ili kuongeza uzalishaji wenye tija katika zao hilo.
Loata Sanare amesema hayo Januari 13 mwaka huu Ofisini kwake wakati wa hafla fupi ya kukabidhi vyeti na zawadi za Pikipiki kwa Maafisa Ugani 10 kati ya 41 ambao wamefanya vizuri katika kuwafundisha wakulima namna bora ya kulima na kuzalisha mahindi kwa ufanisi.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Mhandisi Emmanuel Kalobelo (kulia) akimkabidhi vyeti Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Loata Ole Sanare kwa ajili ya kuwakabidhi Maafisa Ugani waliofanya vizuri katika kuwafundisha wakulima namna bora ya uzalishaji wa zao la mahindi.
Akiwa mgeni rasmi katika hafla hiyo, Loata Sanare amesema kumfundisha mkulima uzoefu wa teknolojia bora ya uzalishaji wa mahindi kutoka nchini China kumesaidia kuongeza uzalishaji wa zao la mahindi kwa gharama ndogo, kuongeza upatikanaji wa chakula na kipato kwa wakulima.
Aidha, Loata Sanare amesema mahindi ni zao la pili ambalo linalimwa kwa wingi baada ya mpunga katika Mkoa wa Morogoro hivyo mradi huo ulikuwa chaguo bora linalogusa idadi kubwa ya wakulima katika Mkoa huo.
Kwa upande wake Balozi wa China hapa nchini Mhe. Wang Ke amezungumzia namna Tanzania na China zinavyoshirikiana katika masuala ya kilimo katika mikoa mbalimbali hapa nchini ukiwemo Mkoa wa Morogoro ambako katika Mkoa huo kuna mashamba ya zao la Mkonge linaloendeshwa na China ambalo baada ya mkonge huo kuvunwa unasafirishwa nchini China ili kuliongezea thamani zao hilo.
Kuhusu mradi wa uzalishaji wa zao la mahindi kwa kutumia Teknolojia kutoka China Balozi Wang Ke amesema mikoa mingine itaiga Mkoa wa Morogoro kutumia teknolojia kutoka China katika kuzalisha mahindi, uzalishaji utaongezeka kwa nchi nzima na hivyo wananchi wake watakuwa na uhakika wa chakula.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Loata Ole Sanare akikabidhi vyeti kwa Maafisa Ugani waliofanya vizuri katika kuwafundisha wakulima namna bora ya uzalishaji wa zao la mahindi
Naye, Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Emmanuel Kalobelo amesema mradi wa kilimo cha mahindi baina ya China na Tanzania uliaza na vijiji viwili vya majaribio ambapo baada ya mafanikio viliongezeka vijiji vingine kumi ndani ya Halmashauri za Mkoa wa Morogoro lengo likiwa ni kuongeza uzalishaji wa mahindi.
Akizungumzia mafanikio ya mradi huo Mhandisi Kalobelo, amesema hadi sasa wamefikia lengo la mradi la kuinua uzalishaji kutoka tani mbili kwa hekta hadi tani tatu kwa hekta.
Sambamba na hayo, Mhandisi Kalobelo amewataka Maafisa ugani kutumia pikipiki hizo kwa malengo yaliyokusudiwa ya kuwatembelea wakulima na kuwafundisha masuala ya kilimo huku akitahadharisha kuwa atakayebainika kukiuka matumizi ya pikipiki hizo atachukuliwa hatua kali za kinidhamu pamoja na kunyang’anywa pikipiki hiyo.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Loata Ole Sanare akikabidhi pikipiki kwa Maafisa Ugani waliokidhi sifa za kupata zawadi hizo za pikipiki
Mdau mkubwa wa mradi huo Erenest Mkongo amesema kabla ya maafisa ugani kupewa pikipiki hizo wakulima zaidi ya 2000 walifikiwa na Maafisa ugani hao, hivyo baada ya kupatiwa vyombo hivyo vya usafiri anatarajia idadi hiyo kuongezeka mara mbili zaidi
Mradi wa kilimo cha mahindi baina ya Tanzania na China ulianza mwaka 2013 kwa Vijiji 2 vya Pea Pea katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa na Mtego wa Simba katika Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro kama vijiji vya mfano ambapo mwaka 2018 vikaanzishwa vijiji vingine 8 katika Halmashauri zote za Mkoa wa Morogoro na kufikia vijiji kumi.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.