Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Mhe. Rebecca Nsemwa amewataka Maafisa Ugani katika Mkoa wa Morogoro kuhakikisha kuwa wanaongeza tija ya uzalishaji kwenye kilimo kwani kwa sasa wamewezeshwa kuwafikia wakulima wengi zaidi hata wale walio maeneo yenye changamoto ya usafiri kwa kuwa Serikali imeowaondolea changamoto hiyo kwa kuwapatia pikipiki.
Mkuu huyo wa Wilaya ametoa kauli hiyo Machi 27 mwaka huu kwenye hafla fupi ya kukabidhi jumla ya Pikipiki 436 kwa Maafisa Ugani Mkoani Morogoro kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Fatma Mwassa, hafla iliyofanyika katika viwanja vya Chuo cha Ujenzi kilichopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.
Mhe. Rebecca amesema anatarajia uzalishaji kwenye Sekta ya kilimo utaongezeka kwa sababu wataalamu hao wa kilimo wataweza kuwafikia wakulima kwa wakati na kutekeleza majukumu yao kwa wakati unaotakiwa.
"...tunauhakika uzalishaji wetu katika maeneo yetu ya kilimo kwa sasa utakwenda kuimarika kwa sababu wataalamu wetu tunauhakika watakwenda kuwafikia au kumfikia mkulima mmoja mmoja..." amesema Mhe. Rebecca Nsemwa.
Ameongeza kuwa Pikipiki hizo 436 watapewa maafisa hao wa kila kata kwenye kila Halmashauri za Mkoa huo.
Aidha, ametumia nafasi hiyo kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa dhamira yake ya dhati ya kukuza sekta ya kilimo hapa nchini.
Kwa upande wake Katibu Tawala Msaidizi upande wa Uchumi na Uzalishaji Dkt. Rozalia Rwegasira wakati akitoa taarifa fupi ya Pikipiki hizo, amesema Pikipiki hizo zimefungwa kifaa maalumu ambacho kinaonesha mahali ambapo Pikipiki hiyo ipo kwa wakati huo, hivyo amewataka Maafisa Ugani hao kuzitumia kwa ajili ya shughuli za kuwafikia wakulima kama ilivyoelekezwa na Wizara ya Kilimo.
Nae Bw. Wanted Mmari ambaye ni Afisa Ugani wa Manispaa ya Morogoro kwa niaba ya Maafisa Ugani wenzake amehaidi kuzitumia Pikipiki hizo kwa uaminifu kama walivyoelekezwa na Wizara ya kilimo.
Amesema kupitia usafiri huo utawasaidia kutekeleza majukumu yao kwa wakati, utafanya kuwafikia wakulima wengi zaidi katika maeneo yao.
Bi. Anna Msamo Afisa Ugani kata ya Mafisa ameishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwakumbuka maafisa ugani hapa nchini.
imeagizwa kuwa pikipiki hizo zitawasaidia Maafisa Ugani kupata takwimu sahihi za wakulima katika maeneo yao pamoja na kuwahudumia bila shida yoyote.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.