Maafisa Ustawi wa Jamii na Maendeleo jamii wametakiwa kuwa na utamaduni wa kufanya ufuatiliaji wa mara kwa mara kweye vituo vya kulelea watoto hususan katika vituo ambavyo havijasajiliwa ili viweze kusajiliwa na kuhakikisha vinafuata miongozo iliyotolewa na Wizara husika namna ya kuendesha vituo hivyo.
Ushauri huo umetolewa Februari 28, 2024 na Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Mipango na Uratibu Mkoa wa Morogoro Bw. Anza Amen Ndosa wakati akifungua kikao cha mapitio ya utekelezaji wa program Jumuishi ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya watoto (PJT MMMAM) chenye lengo la kusimamia uratibu, ufuatiliaji na utekelezaji wa mpango wa huo katika ngazi mbalimabli kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Chief Kingalu katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.
Bwana Ndosa ambaye katika tukio hilo amemwakilisha Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro Dkt. Mussa Ali Mussa, amesema katika vituo hivyo vya kulelea watoto wadogo vihakikishe vinatoa malezi bora kwa kwao na maafisa hao wajenge utamaduni wa kuwatembelea mara kwa mara ili kujionea jinsi vituo hivyo vinavyotoa malezi yanayofaa kwa watanzania.
“…… Kwa hiyo niwaombe tena Maafisa Maendeleo ya Jamii na Maafisa Ustawi wa Jamii kuhakikisha kwamba vituo vyote vya kulelea watoto wadogo vinasajiliwa na vinafuata miongozo iliyotolewa na Wizara ya Elimu katika kuviendesha vituo hivyo….” Amesema Bw. Ndosa.
Katika hatua nyingine Bw. Ndosa amewasisitiza Watendaji hao wa Serikali kushirikiana na viongozi wa dini katika kutoa elimu kwa jamii kupitia mikutano ya hadhara na vyombo vya habari juu ya madhara ya unyanyasaji wa watoto na kuzingatia lishe bora kwa watoto ili waweze kukua vizuri na kuepuka athari ya upungufu wa lishe bora inayopelekea udumavu kwao.
Aidha, Katibu Tawala huyo ameishukuru Serikali inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwajali watoto kwa kuwajengea miundombinu ya Elimu kupitia mradi wa uboreshaji Elimu ya awali na msingi (BOOST) ambao unawasaidia kujifunza wakiwa katika umri mdogo na mazingira mazuri.
Kwa upande wake Mratibu wa Masuala ya Malezi na Ujifunzaji wa Awali kutoka Wizara ya Elimu Dkt. Hawa Juma Seleman amesema mtoto mdogo anatakiwa kupata huduma bora ikiwemo lishe, ujifunzaji wa awali na hatua za makuzi, Afya yenye uwiano na kwamba wadau wakizingatia hayo wataweza kutoa malezi yenye mwitikio chanya.
Naye Bi.Mary Shillah kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wanawake na Makundi Maalumu –Idara ya Watoto, amewataka Watendaji hao wa Serikali kufanya kazi kwa umoja na ushirikiano ili kutoa malezi bora kwa watoto ambapo itasaidia kuondoa mmomonyoko wa maadili katika jamii zinazowazunguka.
Imeelezwa kuwa, Mkoa wa Morogoro una jumla ya vituo 263 vya kulelea watoto wadogo, kati ya hivyo vituo hivyo, vituo 85 pekee ndivyo vilivyosajiliwa kisheria.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.