Maagizo ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa kuhusu ufufuaji wa mashamba ya Mkonge yaliyotelekezwa na Kila Halmashauri kutenga angalau ekari 10 kwa ajili ya vitalu vya zao limeanza kutekelezwa Mkoani Morogoro.
Hayo yamebainishwa Leo Februari 10 mwaka huu baada ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Loata Ole Sanare kuitisha kikao cha Wadaau wa zao la Mkonge kilichofanyika katika Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo na kuwashirikisha wadau mbalimbali wakiwemo wakulima na Uongozi Bodi ya zao la Mkonge Tanzania.
Loata Sanare amewaambia wadau hao kuwa Lengo la kikao hicho ni kuweka mikakati ya kutekeleza maagizo ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano Tanzania aliyoyatoa Mkoani Tanga Januari 20, 2021 na kutaka kila Halmashauri ambazo zimetambulika kustawisha zao la Mkonge kufufua mashamba ya Mkonge huku akitaka halmashauri hizo kutenga japo ekari 10 kwa ajili ya kuandaa vitalu vya zao hilo na kuzigawa bure kwa wakulima.
Aidha, Loata Sanare amesema kikao hicho kitatoa taswira pana ya kuweka mpango kazi wa Mkoa katika kuliendeleza zao la Mkonge huku akitaka kila halmashauri inayolima zao hilo kufufua mazao ya mkonge yaliyotelekezwa, kuendeleza mashamba yanayolima na kuanzisha mashamba mengine mapya kwa ajili ya kustawisha zao hilo.
Maagizo mengine aliyoyatoa Mkuu huyo wa Mkoa ni pamoja na kutaka kuazishwa kwa vyama vya Ushirika vya mazao katika maeneo yanayolima zao hili ili kuwaunganisha wakulima wadogo wanaolima zao la Mkonge ili kurahisisha upatikanaji wa masoko na mitaji katika kukuza kilimo cha zao hilo.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Mhandisi Emmanuel Kalobelo akimkaribisha Mkuu wa Mkoa kufungua kikao hicho aliwaeleza wajumbe wa kikao hicho kuwa zao la Mkonge hapo awali lilikuwa linalimwa katika Halmashauri mbili tu za Kilosa na Morogoro.
Hata hivyo baada ya kufanyika uhamasishaji wa kutosha kutoka kwa Viongozi wa Serikalingazi ya Taifa, hivi sasa halmashauri za Gairo na Mvomero nazo zimeamua kulima zao hilo.
Aidha, Mhandisi Kalobelo amesema kwa sasa Mkoa una jumla ya mashamba sita yenye jumla ya ukubwa wa hekta 19,834 ambapo kati ya hizo hekta 7,573 zinalimwa sawa na 38% huku akiwatambulisha wakulima wadogo 14 wenye mashamba yenye ukubwa wa jumla ya hekta 245.
Mhandisi Kalobelo amebainisha shughuli zilizofanywa na Mkoa katika kutekeleza agizo la Serikali la kufufua zao la Mkoange, kuwa ni pamoja na kutambua mashamba yasiyoendelezwa mfano katika Wilaya ya Morogoro, jumla ya mashamba sita yenye ukubwa wa hekta 1,923 yamebainika na wamiliki wamepatiwa notisi ya siku 90 hadi februari 28, mwaka huu wawe wameonesha nia ya kuyaendeleza la, yatatwaliwa na kugawanywa kwa wananchi ili kulima zao la Mkonge.
Hatua nyingine iliyofanyika ni kutoa mafunzo kwa wataalamu wa kilimo, mafunzo yanayohusu kilimo cha mkonge ili waweze kutoa huduma ya ugani kwa wakulima kitaalamu zaidi, mafunzo hayo ya siku mbili yalitolewa na watafiti kutoka Mlingano na shughuli ya tatu ni uanzishwaji wa vitalu vya miche kupitia Halmashauri, mfano Halmashauri ya Gairo na Morogoro zimeazisha vitalu vya miche ya zao la Mkonge 32,000.
Nao wadau wa kikao hicho akiwemo cyriacus Faustine Ndyamkama kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo cha SUA alitaka vijana washirikishwe kikamilifu katika mkakati wa kufufua zao la Mkonge ili katika ushiriki wao waweze kupata faidika kutokana na kilimo cha zao hilo badala ya vijana wengi kwa sasa kuishia kufanya shughuli muda mfupi na hazina tija kubwa ikiwemo shughuli ya uuzaji wa laini za simu.
mwisho
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.