Madaktari Bingwa wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan wamedhamiria kutoa huduma ya afya kwa siku sita katika Halmashauri zote za Mkoa wa Morogoro kuanzia Oktoba 14 hadi 20 Mwaka huu.
Hayo yamesemwa Oktoba 14, 2024 na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Adam Kighoma Malima wakati akizungumza na Madaktari hao watakao toa huduma za kibingwa na bobezi katika Halmashauri zote za Mkoa huo na kuwajengea uwezo wataalamu wa afya waliopo katika hospitali zilizopo katika Halmashauri hizo.
Mhe. Malima amewasisitiza Madaktari hao kutoa hamasa kwa wananchi kuwa na utamaduni wa kupima afya mara kwa mara ili kujua hali za afya zao kwani itasaidia wananchi kujitambua mapema hasa kwa magonjwa yasiyo ya kuambukiza na kuanza uchunguzi mapema ili kuanza matibabu mapema.
"...nawashukuru sana kwani huduma ya afya mtakayokwenda kutoa kwenye Halmashauri zetu ni huduma muhimu sana kwa Jamii nendeni mkawasaidie wananchi..." amesema Mhe. Adam Kighoma Malima
Aidha, Mhe. Adam amewataka wananchi kuwa na utamaduni wa kutumia lishe bora na sahihi kwa watoto wadogo, vijana na wazee kwani lishe bora ni mlo wenye virutubisho sahihi ambavyo haviwezi kuharibu afya ya mtu kwa kufuata maelekezo ya wataalamu wa lishe wanavyoelekeza ili kuwa na afya imara.
Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa Mkoa amewataka wananchi kuendelea kujiandikisha kwenye orodha ya wapiga kura wa Serikali za Mitaa ili kuweza kupata fursa ya kupiga na kupigiwa kura ifikapo Novemba 27 Mwaka huu na kuweza kupata kiongozi bora kwa maendeleo ya Jamii na Taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake, Mratibu wa Madaktari bingwa wa Rais Samia Mkoa wa Morogoro kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Ismail Mtitu amesema kila Halmashauri za Mkoa huo itapokea madaktari bigwa 6 na muuguzi 1 kuanzia Oktoba 14 hadi 20 Mwaka huu ambao watatoa huduma za kibingwa kwa siku 6.
Sambamba na hayo, Mratibu huyo amesema Madaktari hao wataendelea kusimamia na kusaidia huduma za kibingwa zinatolewa kikamilifu, kuwajengea uwezo Madaktari husika wa hospitali zilizopo katika Halmashauri hizo na kusaidia hospitali kuanzisha wodi maalum za watoto wachanga.
Mwisho.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.