Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Bw. Ismail Ali Ussi amempongeza Mganga Mkuu wa hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Morogoro Dkt. Daniel Nkungu pamoja na wahudumu wengine wa hospitali hiyo kwa utendaji kazi wao mzuri na jitihada wanazotoa katika kuwahudumia wagonjwa hospitalini hapo na kuelezwa kwamba wanaitendea haki taaluma yao.
Pongezi hizo zimetolewa na kiongozi huyo Aprili 12, 2025, wakati wa uzinduzi wa jengo la wagonjwa wa nje pamoja na ofisi za utawala, lenye thamani ya zaidi ya Shilingi milioni 505, lililopo katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro.
Aidha, Kiongozi huyo amewataka watumishi wa sekta ya afya kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi kwani amesema Serikali imeweka mikakati madhubuti ya kuboresha mazingira rafiki kwa wagonjwa na watumishi, sambamba na kuboresha miundombinu ya utoaji huduma katika sekta ya afya.
Katika hatua nyingine, Bw. Ussi ametoa shukrani kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa juhudi zake za kuboresha miundombinu mbalimbali, ikiwemo sekta ya afya, ili kutatua changamoto zilizokuwa zikiwakabili wananchi wa Mkoa huo.
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Morogoro Mjini, Mhe. Abdul Aziz Abood, amesema jengo hilo limeongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za afya kwa sababu hiyo huduma afya kwa wananchi wa morogoro imeimarika na hakuna haja ya wagonjwa wengi kupelekwa Dar es Salaam au Dodoma kufuata huduma ya afya kwa kuwa vipimo vyote muhim vipo katika hospitali hiyo ikiwemo kipimo cha CT Scan.
Mwisho
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.