Maafisa Biashara na Utamaduni ngazi ya Mkoa na Halmashauri Mkoani Morogoro wamepatiwa Mafunzo ya namna ya kuunganisha Mfumo wa AMIS NA TAUSI (PPT) unaolenga kukusanya taarifa za wasanii pia kuimarisha makusanyo ya mapato ya shughuli za Biashara, Sanaa na Utamaduni katika Halmashauri zao.
Hayo yamebainishwa leo Mei 21, 2025 na Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Muziki Baraza la Sanaa Taifa (BASATA) Bw. Kelvin Stanslaus wakati wa kikao kazi cha Maafisa hao kilichofanyika Chuo Kikuu cha Cha Sokoine (SUA) ambapo zaidi ya wataalamu 25 wamehudhuria kikao hicho.
".. leo tunafanya mafunzo ya mfumo wa AMIS NA TAUSI ambapo lengo lake ni kukusanya taarifa za wasanii na kukusanya mapato.." amesema Bw. Kelvin Stanslaus
Kiongozi huyo amesema mfumo wa AMIS NA TAUSI ni mfumo wa wadau wa sanaa unaotumiwa na (BASATA) Kwa ajili ya usajili na kutoa vibali vya wasanii na wadau hao wa sanaa pia kusaidia katika kukusanya mapato katika shughuli za kisanaa kama vile kumbi za starehe, wasanii wadodogo na wafanyabiashara wanaomiliki kazi za sanaa.
Kwa upande wake Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi kutokea Baraza la Sanaa Tanzania ( BASATA) Dkt. Gervas Kasiga amesema kuunganishwa kwa Mfumo wa AMIS NA TAUSI na mifumo mingine utaenda kuleta mapinduzi makubwa katika ukusanyaji wa mapato ya sekta ya sanaa ambapo awali sekta hiyo ilikuwa ilikuwa haina mchango wowote hivyo kutokana na mfumo huo Serikali itaenda kupata mapato kwa ngazi zote hivyo BASATA kujiendesha kutokana na mapato yatokanayo na kazi za kisanaa.
Naye Afisa Utamaduni Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Bi. Paula Patriki ameishukuru Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia BASATA kwa kuwaletea mafunzo hayo ambayo yatawajengea uwezo katika utendaji kazi wao pia kusimamia wasanii na mapato yatokanayo na shughuli za Kisanaa ngazi za halmashauri, Mkoa na Taifa.
Naye Kaimu Afisa Utamaduni Mkoa wa Morogoro Bi. Grace Njau amesema Mfumo huo utaenda kuwasaidia maafisa hao katika kukusanya mapato kwa urahisi kupitia tasinia hiyo ya sanaa hivyo kuondokana na Rushwa ambapo kwa sasa shughuli zote za kifedha zikiwemo usajili zitafanyika kupitia mfumo wa kieletroniki.
NWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.