Washiriki wa Sensa ya Watu na Makazi wafundwa
Washiriki wa Sensa ya watu na Mkazi ngazi ya Mkoa Mkoani Morogoro wanaoendelea kunolewa kwa siku 21, wametakiwa kuwa wazalendo pindi watakapokwenda kutoa mafunzo hayo kwa Makalani wa Sensa katika ngazi za Wilaya.
Baadhi ya Washiriki wa Sensa ya watu na Mkazi ngazi ya Mkoa Mkoani Morogoro wakiendelea na mafunzo yao yanayofanyika katika kituo cha kutolea Elimu ya watu wazima (WAMO) Mkoani humo.
Rai hiyo imetolewa na Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa morogoro Mhandisi Ezron Kilamuhama alipowatembelea washiriki hao kwa lengo la kuangalia maendeleo ya mafunzo hayo yanayofanyika Kituo cha kutolea Elimu ya Watu Wazima (WAMO) kilichopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.
Akiwa katika eneo la mafunzo Mhandisi Ezron Kilamuhama amesema zoezi la Sensa ya watu na Makazi hufanyika mara moja kila baada ya miaka 10, kwa sababu hiyo washiriki wanatakiwa kuwa makini katika kufundisha walio chini ambao ni ngazi ya Wilaya.
Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro, Mhandisi Ezron Kilamuhama akizungumza na Washiriki wa Sensa ya watu na makazi (Hawapo Pichani).
Amebainisha kuwa endapo kutakuwa na makosa yoyote yatakayofanyika katika sense ya mwaka huu na kwa kuwa sense hufanyika kila baada ya miaka kumi basi makosa hayo yataathiri taifa na wananchi wake kwa miaka kumi ijayo, hivyo pamoja na changamoto zozote zitakazojitokeza wakati wa zoezi hilo ni budi watangulize nidhamu na Uzalendo kwa taifa lao.
“lakini pamoja na hayo niwaombe sana kwa sababu kama nilivyotangulia kusema lina umuhimu wa kipekee na ni zoezi la kitaifa, lazima tujitahidi sana kuwa walimu, tulifanye kwa nidhamu kubwa sana lakini pia tulifanye kizalendo” amesisitiza Mhandisi Kilamuhama.
Hata hivyo, amesema sense ya mwaka huu ni ya kipekee ukilinganisha sensa ya miaka mingine kwa kuwa sensa ya mwaka huu kwanza ni inafanyika kidijitali lakini pia inahusisha Makazi na ndio maana imetanguliwa na zoezi la Anwani za Makazi na Posti kodi ambapo Mkoa wa Morogoro ulitekeleza zoezi hilo kwa 106% ya lengo, jambo ambalo litarahisisha sana zoezi lote la Sensa ya watu na Makazi.
Mmoja wa wawashiriki wa mafunzo ya Sensa ya watu na makazi akijikumbusha namna ya kutumia zana ya kukusanyia Takwimu kidijitali (Kishikwambi) kitakacho tumika wakati wa Sensa hiyo.
Naye Mratibu wa Sensa Mkoa wa Morogoro Bw. Charles Mtabo amesema mafunzo hayo ya sensa ngazi ya Mkoa yanahusisha washiriki takribani 416 na yameanza Julai 6 na yatakamilika Julai 26, 2022 na baada ya kukamilika wataanza ngazi ya tatu ya mafunzo hayo ya sensa ambayo ni ya ngazi ya Wilaya.
Mratibu wa Sensa ya watu na Makazi Mkoa wa Morogoro Bw. Charles Mtabo.
Kwa upande wake Roda Sheba ambaye ni mshiriki, amesema madhumuni ya Serikali kuwa na sensa ya watu na Makazi ni kupata takwimu sahihi zitakazosaidia serikali kupanga mipango yake ya kuwahudumia wananchi,hivyo akatoa wito kwa wananchi, kwanza kujiandaa kushiriki sensa hiyo lakini pia kutoa takwimu zilizo sahihi huku akitoa rai kwa washiriki wenzake kuwa wazalendo wakati wote wa zoezi la Sensa.
Roda Sheba ambaye ni mmoja wa washiriki wa Sensa ya watu na makazi Mkoa wa Morogoro ametoa wito kwa washiriki wenzake kuwa wazalendo wakati wote wa zoezi hilo.
Sensa kwa maendeleo, jiandae kuhesabiwa
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.