Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, TAMISEMI Sehemu ya Miundombinu Mhandisi Rogatus Mativila amewataka Makatibu Tawala Wasaidizi wa Sekretarieti za Mikoa hapa nchini kusimamia kwa karibu utekelezaji wa miradi ya maendeleo ili miradi hiyo kuwa na ubora na thamani tarajiwa kwa manufaa ya Taifa.
Mhandisi Rogatus amesema hayo hivi karibuni wakati wa kikao cha Makatibu Tawala Wasaidizi wa Mikoa Sehemu ya Miundombinu na Ofisi ya Rais Tamisemi kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Mkandarasi House Jijini Dodoma kwa lengo la kujadili mambo muhimu yanayohusu kazi za ujenzi, ukarabati na matengenezo ya miundombinu katika Mikoa 26 ya hapa nchini.
"...ni lazima kuhakikisha yafuatayo, moja kusimamia miradi kwa mujibu wa mikataba, pili kuwa na mpango wa usimamizi wa muda mrefu, wa kati na mfupi na tatu kuepuka upendeleo ndani ya watumishi..." amesema Mhandisi Rogatus Mativila
Aidha, Naibu Katibu huyo amewasisitiza Makatibu Tawala Wasaidizi hao kusimamia miradi bila upendeleo na kuhakikisha inaisha kwa wakati na kwa ufanisi ili kusogeza huduma karibu na wananchi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Makatibu Tawala Wasaidizi wa Sehemu ya Miundombinu Kote nchini Mhandisi Ezron Kilamhama kutoka Mkoa wa Morogoro, kwa niaba ya Makatibu Tawala Wasaidizi wenzake alimuahidi Naibu Katibu Mkuu huyo kuwa wamepokea maagizo hayo na kukiri kusimamia miradi kwa ufanisi kwa kushirikiana na wakandarasi ili kupata ubora unaohitajika katika miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo yao.
Naye, Katibu wa Makatibu Tawala Wasaidizi hao Mhandisi Arch Chagu kutoka Mkoa wa Mwanza amesema ndani ya Mwezi huu wa Februari, watapeleka mpango kazi wao Ofisi ya Rais, TAMISEMI ili kuwathibitishia viongozi wao namna walivyojipanga kwenda kutekeleza maagizo ya Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI aliyoyatoa.
Mwisho.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.