Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Malima amemuagiza Meneja wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) pamoja na Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoani humo kusimamia miradi kwa karibu miradi inayotekelezwa Mkoani humo ili iweze kukamilika kwa wakati na kwa ubora unatakiwa.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Malima akizungumza na wadau wa sekta ya nishati wakati wa kikao cha kupokea taarifa ya ya REA na TANESCO.
Mhe. Malima ametoa agizo hilo Julai 24 mwaka huu wakati wa kikao cha kupokea taarifa ya utekelezaji wa miradi ya REA na TANESCO Mkoani humo, kilichofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro.
Mhe. Adam Malima amesema, Serikali imetoa fedha nyingi za kutekeleza miradi ya usambazaji umeme katika Mkoa huo ili kuondoa changamoto ya upatikanaji wa umeme kwa wananchi wake jambo ambalo bado linakwamishwa na wakandarasi wachache kutofikia malengo hayo.
Kwa sababu ya wakandarasi hao kuchelewesha kukamilika kwa miradi hiyo kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa inapelekea wananchi kuitupia lawama Serikali yao, hivyo ameagiza viongozi wa REA na TANESCO Mkoa wa Morogoro kuwasimamia wakandarasi kukamilisha miradi hiyo.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe Adam Malima akiwa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Mussa Ali Mussa wakati wa kikao.
“...hebu tuangalie hili suala la monitoring and supervision kwa wakandarasi wetu ili pale ambapo serikali imepeleka fedha na miradi inatakiwa kukamilika kwa wakati basi ikamilike...” amesema Mkuu wa Mkoa.
Akitolea mfano Mkandarasi M/s HNXJDL JV ambaye anatekeleza mradi usambazaji umeme vijijini wenye thamani zaidi ya shilingi bilioni 26 katika Wilaya za Kilosa, Mvomero na Gairo miradi 78 iliyotakiwa kukamilika Disemba 2022 lakini hadi sasa Mkandarasi huyo amewasha umeme katika vijiji 27 pekee, hivyo ameongezewa muda hadi Disemba 2023 kukamilisha vijiji vilivyobaki hali ambayo bado inaleta wasiwasi kama atakamilisha miradi yote kwa huo uliobaki.
Sambamba na hilo, Mkuu huyo wa Mkoa amewataka Meneja wa REA na TANESCO Mkoani humo kushirikiana na Jeshi la Polisi kudhibiti wizi wa miundombinu ya umeme katika Mkoa huo ikiwemo mafuta ya Transifoma na nyaya za shaba.
Pamoja na kushirikiana na Jeshi hilo, Mkuu wa Mkoa amemwagiza Meneja wa TANESCO kutafuta mbinu mbadala za teknolojia za kisasa za kuwakamata wezi wa miundombinu ya umeme ikiwa ni pamoja kuwa na vifaa vinavyorekodi matukio hayo katika maeneo mbalimbali hususan yaliyokithiri matukio hayo.
Naye, Meneja wa TANESCO Mkoani Morogoro Mhandisi Fadhili Chilombe ameeleza mikakati ya Shirika hilo ya kuhakikisha Mkoa wa Morogoro unaondoa au kupunguza changamoto ya upatikanaji wa umeme ndani ya Mkoa huo.
Miongoni mwa mikakati hiyo ni pamoja na kununua transifoma mpya ya MV 120 ambayo itazalisha umeme Megawati 102 na kwamba kwa sasa wapo katika hatua ya ufungaji wa transifoma hiyo katika kituo cha kupoozea umeme cha Msamvu na wanatarajia kazi hiyo kukamilika ifikapo Oktoba 31 mwaka huu, hivyo changamoto ya kukatika umeme katika Manispaa ya Morogoro itapungua.
Meneja wa TANESCO Mkoa wa Morogoro Mhandisi Fadhili Chilombe akielezea mikakati ya shirika hilo ndani ya Mkoa huo.
Ameongeza kuwa shirika la TANESCO limetenga Bilioni 4.6 kwa ajili ya matengenezo ya njia za kusambaza umeme pamoja ununuzi wa nguzo za zege 551 kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya umeme.
Kwa upande wake Mhandisi wa Miradi ya REA Mkoani Morogoro, Bi. Aneth ameeleza changamoto zinazoikabili REA katika majukumu yake zikiwemo idadi ya wananchi wanaojitokeza kuunganishwa ni ndogo japokuwa bei ni 27,000 katika maeneo ya vijijini, changamoto ya miundo mbinu ya barabara katika baadhi ya Wilaya hivyo kusababisha ucheleweshwaji wa vifaa.
Meneja miradi ya REA Mkoa wa Morogoro Mhandisi Aneth Malingumu akiwasilisha taarifa ya miradi ya REA inayotekelezwa Mkoani humo.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.