Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango amezitaka kampuni zinazoagiza mbegu kutoka nje ya nchi kuzalisha mbegu hizo hapa nchini kutokana na tija ndogo inayopatikana kupitia sekta ya kilimo na kuitaka Wizara ya Kilimo kusimamia utekelezaji wa maelekezo hayo.
Kauli hiyo ameitoa Mei 27, 2021 wakati akihitimisha maadhimisho ya kumbukizi ya 17 ya hayati Edward Moringe Sokoine yaliyofanyika Mkoani Morogoro katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo – SUA ambapo alikuwa mgeni rasmi wa maadhimisho hayo.
‘’Ninazitaka kampuni zote zinazoagiza mbegu kutoka nje zizalishe mbegu hizo hapa nchini na Wizara ya Kilimo ijipange kusimamia na kufuatilia utekelezaji wa maelekezo haya, taasisi zetu za Magereza na JKT lazima zijizatiti zaidi katika uzalishaji wa mbegu’’ Amesema Dkt. Mpango.
Dkt. Mpango amesema kutokuwepo kwa hatua madhubuti za kuinua sekta ya kilimo kumepelekea kushindwa kushawishi viongozi, vijana na wasomi kujikita katika kilimo biashara na kutofanikiwa kuzishawishi taasisi za kifedha kutoa mikopo yenye riba nafuu katika sekta ya kilimo.
Katik hatua nyingine, Dkt. Mpango ameitaka Wizara ya Kilimo na Mifugo kufikisha huduma za ugani kwa wakulima vijijini na kusimamia mfumo mzima wa vitendea kazi kuwafikia wakulima hao ili kuwanufaisha na kilimo hicho.
Kwa upande wake Mkuu wa Chuo hicho Jaji Mstaafu Joseph Warioba amebainisha lengo mahususi la kuanzishwa kwa Chuo hicho ni kufanya tafiti na kuwajenjea uwezo wanafunzi kujitegemea kwa kupiga vita umasikini na kutoa huduma zinzohitajika kwenye kilimo kwa wananchi wa vijijini.
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Martine Shigela amesema atashirikiana vizuri na SUA katika kukuza uzalishaji wa kilimo kwa kutimiza zima ya Serikali ya Mkoa huo kuwa ghala la chakula kwa kufanya mapinduzi ya sekta ya kilimo na kuenzi mazuri ya hayati Moringe Sokoine.
Hayati Moringe Sokoine alifarikii Aprili 12, 1984 eneo la Dakawa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero Mkoani Morogoro, ambapo kumbukizi ya mwaka huu inatimiza miaka 37 tangu kufariki kwake ikibebwa na kaulimbiu ‘’ Teknolojia za Kilimo, Tija na Ushindani katika Soko: Tanzania kuelekea Nchi ya Uchumi wa Kati wa Juu.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.