Wananchi wa Wilaya za Mlimba na Morogoro Vijijini Mkoani Morogoro wameshauriwa kutumia nyuzi zinazotokana na mashina ya migomba kama chanzo cha kujipatia kipato ndani ya familia na kuinua mapato ya halmashauri hizo kwa kutumia nyuzi za migomba kutengeneza vifaa mbalimbali, kuviuza na kuratibu fursa hiyo kuwa ajira kwa vijana.
Ushauri huo umetolewa Juni 20, 2024 na Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Alhaji Dkt. Mussa Ali Mussa wakati wa Kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba na halmashauri ya Wilaya ya Malinyi wakati wa kujadili hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) baada ya kupewa nafasi ya kutoa salamu katika vikao hivyo.
Amesema, Migomba imekuwa hatumiki kwa chochote katika halmashauri hizo ambazo zina utajiri mkubwa wa zao hilo bila kujua kuwa migomba hiyo ni utajiri uliopindukia kwa kuwa inatoa nyuzi zinazoweza kutengeneza vifaa mbalimbali vikiwemo vikapu, mikoba, mikeka, vitambaa na hata taulo za kike.
“Tuliloligundua na wataalamu wangu, migomba ni utajiri uliopindukia na tukijipanga vizuri utaweza kusaidia kunyanyua mapato..” amesisitiza Dkt. Mussa.
Kwa sababu hiyo, Katibu Tawala huyo amezishauri Halmashauri za Morogoro DC na Mlimba na Maeneo mengine yanayostawisha zao hilo kutotupa migomba hiyo badala yake wachangamkie fursa hiyo kuitumia kama moja ya chanzo cha kukuza mapato ya Halmashauri na kukuza Uchumi wa jamii inayowazunguka.
Aidha, Dkt. Mussa Ali Mussa amebainisha kuwa mashine inayotumika kutengeneza bidhaa hizo zinazotokana na migomba ikiwemo mikoba, vikapu, mikeka, nguo n.k. kwa kutumia nyuzi zake inapatikana Chuo cha Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi - VETA Mikumi, Wilayani Kilosa Mkoani Morogoro kwa bei ndogo ya shilingi 1.2 Mil.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.