Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa akizungumza wakati wa kilele cha Maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani 2023 yaliyofanyika Kitaifa Mkoani Morogoro.
Matokeo ya awali ya utafiti wa viashiria vya UKIMWI 2022/2023 nchini yamezinduliwa leo Disemba Mosi na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb) ikiwa ni kilelel cha Maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani ambayo kitaifa yamefanyika Mkoani Morogoro.
Mhe, waziri Mkuu amezindua matokeo hayo leo Disemba Mosi, 2023 akiwa mgeni rasmi kwenye maadhimisho hayo ya siku ya UKIMWI Duniani yaliyofanyika katika viwanja vya Morogoro Sekondari katika halmashauri ya manispaa ya Morogoro.
Akizindua matokeo hayo ya utafiti huo Mhe. Kassim Majaliwa amesema matokeo ya awali yanaonesha kuwa Tanzania imepiga hatua katika mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI, lakini harakati za kuutokomeza ugonjwa huo bado zinaendelea.
Aidha, Mhe. Waziri Mkuu amesema utafiti huo unaonesha wanawake wamejitokeza kwa wingi zaidi katika upimaji wa VVU huku wanaume wakiwa nyuma, hivyo ametumia fursa hiyo kuwataka wanaume hapa nchini kuwa mstari wa mbele katika kupima VVU.
“...na matokeo ya awali ya utafiti huo ambayo pia nitayazindua hivi punde yameonesha kuwa nchi yetu imepata mafanikio makubwa katika mapambano dhidi ya UKIMWI...lakini malengo ya kutokomeza kabisa hayajafikiwa...” amesema Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.
Aidha, utafiti huo umeonesha kuwa watu wanaoishi na VVU kwa watu wenye umri zaidi ya miaka 15 ni asilimia 4.4, kwa kigezo cha jinsia utafiti umeonesha wanawake ni asilimia 5.6 ikilinganishwa na asilimia 3.0 kwa wanaume, kigezo cha makazi mijini asilimia 4 na vijijini asilimia 4.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa akiwa pamoja na viongozi wakiwemo Mawaziri, Manaibu Mawaziri, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima na Wadau wa kudhibiti UKIMWI nchini na nje ya nchi wakati wa kilele cha Maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani 2023.
Sambamba na hilo utafiti huo ummeonesha kuwa hali ya maambukizi kwa watu walio zaidi ya miaka 15 yamepungua kutoka watu 72000 mwaka 2016/2017 hadi kufikia watu 60000 mwaka 2023.
Baadhi ya Wakuu wa Wilaya za Mkoa wa Morogoro wakiwa kwenye sherehe za Maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani 2023.
Aidha, utafiti umebaini kuwa kiwango cha kufubaza VVU kimeongezeka hadi kufikia asilimia 78 ambapo kwa wanawake ni asilimia 80.9 wanaume ni 72.2 ukilinganisha na asilimia 52 ya utafiti wa 2016/17. Katika hatua nyingine Waziri Mkuu huyo amehimiza wananchi kubadili mitindo ya maisha ambayo yanachochea kwa kiasi kikubwa kuongezeka kwa maambukizi ya VVU na UKIMWI.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa akipokea maandamano wakati wa kilele cha Maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani yaliyofanyika Kitaifa Mkoani Morogoro.
Kwa upande wake Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu (Mb) amemshukuru Waziri Mkuu kwa kuwa balozi wa kuhamasisha wanaume kupima VVU hapa nchini ambapo imesaidia wanaume wengi kujitokeza kupima kujua hali zao za maambukizi.
Aidha, amesema Serikali kupitia Wizara ya Afya itaajili wahudumu wa Afya ngazi ya jamii 137000 ifikapo Janauari 2024 lengo ni kuendelea kutoa huduma za VVU na UKIMWI karibu na wananchi. Hata hivyo ameongeza kuwa Novemba 24, 2023 Wizara ilizindua Mpango wa Taifa wa kudhibiti UKIMWI, Magonjwa ya Ngono na homa ya Ini.
Nao watu waishio na Virusi vya UKIMWI kupitia kwa Mwenyekiti wa Baraza la Watu waishio na Virusi vya UKIMWI – NACOPHA Bi. Leticia Moris ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kuanzisha mpango wa Bima ya Afya kwa Wote na kuiomba Wizara kuhakikisha kuwa mpango huo unafanikiwa kwani utawasaidia watu waishio na VVU kupata huduma za Afya bila usumbufu.
Maadhimisho hayo ya Siku ya UKIMWI Duniani 2023 yanaenda sambamba na kaulimbiu isemayo “Jamii iongoze kutokomeza UKIMWI”
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.