Mashindano ya mbio za magari yaliyozinduliwa leo Mkoani Morogoro yanatarajia kwenda kuutangaza Utajiri wa Mkoa huo hususan utalii wa mbuga za Wanyama, milima ya Udzungwa na utajiri mwingine uliopo ndani ya Mkoa huo.
Hayo yamebainishwa leo Septemba 19, 2025 na Waziri mwenye dhamana ya Michezo, Sanaa na Utamaduni Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi wakati akifungua mashindano hayo katika viwanja vya Kiwanda cha Tumbaku cha Mkwawa Leaf Mkoani Morogoro.
Amesema, mashindano hayo ya mbio za Magari yanayojulikana kama Mkwawa Rally of Tanzania (African Rally of Championship) yanakwenda kutoa mchango mkubwa katika kuutangaza Utalii wa Mkoa wa Morogoro hivyo kukuza Uchumi wake na wa Taifa la Tanzania.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amesema, Mkoa wa Morogoro una vigezo lukuki vya kuwa mwenyeji wa mashindano hayo ikiwa ni Pamoja na uzuri wa mazingira yanayovutia, Usalama na uwezo wake kuratibu matukio makubwa kama hayo.
Aidha, ameishukuru Serikali kwa kuunga mkono na kuuendeleza mchezo huo huku akiwashukuru wananchi wa Morogoro kushiriki uzinduzi wa mbio hizo za magari na ametumia fursa hiyo kuliomba Shirikisho la mchezo huo Duniani, kuuleta tena mchezo Mkoani humo na kuahidi kuwa watajipanga na kufanya vema zaidi kuliko mwaka huu.
“Tumeongea nao watu wa shirikisho ili mwakani wailete tena tujipange na kuwa kitu kikubwa kwa hapa Morogoro na kwa Tanzania” amesisitiza Mhe. Adam Malima.
Naye Yohana Emmanuel Manu kwa niaba ya wananchi wa Mkoa huo amesema, mashindani hayo yanaleta hamasa, umoja na Ushirikiano miongoni mwa watanzania na ndugu zetu wa nchi Jirani, lakini pia amesema mashindano hayo yanaongeza watalii hivyo kukuza Uchumi wa mtu mmoja mmoja kupitia bidhaa wanazouza na kuongeza mzunguko wa fedha ndani ya mkoa.
Mashindano hayo ya African Rally of Championship yatafanyika kwa siku tatu kuanzia Septemba 19 hadi Septemba 21, 2025 na kushirikisha wanamichezo kutoka nchi za Kenya, Unganda, Rwanda India na wenyeji Tanzania.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.