Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro Dkt. Mussa Ali Mussa amesema Ofisi yake itamchukulia hatua za kinidhamu Meneja wa Wakala ya Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) Wilaya ya Kilombero kwa kutosimamia kikamikifu ujenzi wa barabara ya Kibaoni – Nanganje kwa kiwango cha lami yenye urefu wa mita 900 baada ya muda wa kukamilisha ujenzi huo kupita.
Dkt. Mussa ametoa agizo hilo Oktoba 4 mwaka huu alipotembelea mradi huo kuona hatua iliyofikiwa wakati wa ziara yake ya siku moja ya kukagua miradi ya barabara katika Wilaya za Kilombero na Ulanga.
Amesema, Serikali imetoa zaidi ya shilingi milioni 400 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo, na muda wa kukamilika ilikuwa Septemba 30, 2023 kwa sababu hiyo Meneja huyo anapaswa kuchukuliwa hatua kwa kile alichokiita ni uzembe katika kutekeleza majukumu yake.
"...kuna haja ya kuwachukulia hatua wahusika wa TARURA kwa sababu wao ndiyo waliomtafuta mkandarasi, wao ndiyo waliosimamia... na barabara yenyewe haifiki hata kilometa moja na fedha zipo, kila kitu kipo lakini bado barabara haijamalizika...” amesema Dkt. Mussa.
Aidha, Katibu Tawala huyo amemtaka Meneja huyo wa TARURA kuhakikisha kuwa kazi zake anazozisimamia zinakamilika kwa wakati na kwa kiwango kinachotakiwa kulingana na fedha iliyotolewa ili kuwasaidia wananchi watakaotumia barabara hiyo kuondokana na changamoto ya ubovu wa barabara.
Naye, Katibu wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Morogoro Ndg. Solomon Kasaba amesema ucheleweshaji wa miradi ya barabara inasababisha wananchi kuitupia lawama Serikali na chama cha CCM kuwa haifanyi kazi, wakati kuna watu wachache tu ndiyo kikwazo cha kugombanisha wananchi na Serikali yao huku akishauri TARURA kuchukua wakandarasi wenye sifa ili kukidhi mahitaji ya miradi husika.
Kwa upande wake Meneja wa TARURA Wilayani Kilombero Mhandisi Kalume amesema sababu ya kutokukamilika kwa wakati kwa mradi huo ni pamoja na kuchelewa kupatikana kwa msamaha wa kodi, mvua hasa kipindi cha masika, pamoja na uwezo mdogo wa kifedha wa mkandarasi anayejenga barabara hiyo.
Ujenzi wa barabara hiyo ya Kibaoni - Nanganje utakaogharimu shilingi mil.400 hadi kukamilika kwake umefikia asilimia 60, na mkandarasi ameshalipwa shilingi Mil. 200.
MWISHO.
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.