Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Fatma Mwassa ameagiza uongozi wa shule ya Green City iliyopo katika Manispaa ya Morogoro kumsimamisha kazi Bwana Henri Wadelanga (60) kwa kosa la kumpiga hadi kupoteza fahamu mwanafunzi Asia Haidari Sharifu wa kidato cha tano mchepuo wa HGK katika shule hiyo.
Mhe. Fatma Mwassa ametoa agizo hilo Januari 10 mwaka huu alipotembelea shule hiyo kwa ajili ya kutoa uamuzi na kuzungumza na walimu pamoja na wanafunzi wa shule hiyo.
Mkuu huyo wa Mkoa amesema Bwana Henri Wadelanga amefanya makosa mbalimbali yakiwemo kumpiga mwanafunzi hadi kupoteza fahamu, kinyume na sheria kwa kuwa yeye sio mwalimu hivyo haruhusiwi kupiga wanafunzi.
Sambamba na hilo, Mkuu wa Mkoa amemuagiza Afisa Elimu Mkoa wa Morogoro kwa kushirikiana na Mganga Mkuu wa Mkoa kumpeleka mwanafunzi huyo Hospitali ya Rufaa ya Mkoani hapa ili kubaini kama amepata athari nyingine za kiafya zilizotokana na kipigo hicho.
Akithibisha kutokea kwa tukio hilo Afisa Elimu Mkoa wa Morogoro Bi. Germana Mung'aho amesema tukio hilo limetokea tarehe 8 Januari mwaka huu majira ya saa tatu usiku ambapo Meneja huyo alikuwa anawapokea wanafunzi waliotoka likizo.
Afisa Elimu huyo ameongeza kuwa Ndugu Henri Wadelanga alichukua hatua hiyo ya kumpiga mwanafunzi huyo kwa madai ya kwamba alitukanwa na mwanafunzi huyo.
Aidha ameongeza kuwa tukio Hilo limeshafunguliwa jarada (Morogoro RB No. 228/2023) katika kituo Kikuu cha Polisi Mkoani Morogoro na mtuhumiwa anashikiliwa na vyombo vya dola kwa hatua zaidi za kisheria.
Sambamba na hilo Bi. Germana Mung’aho ametoa wito kwa walimu juu ya utoaji wa adhabu kwa wanafunzi kwa kufuata Waraka wa Elimu kuwa hauruhusu mwanafunzi kupigwa maeneo mbalimbali ya mwili wake, na adhabu ya viboko ndiyo adhabu kubwa inayotambulika.
Aidha Waraka huo wa Elimu umewataka walimu kutoa adhabu ya viboko isiyozidi vinne na lazima Mwalimu Mkuu au Mkuu wa shule aidhinishe na iwekwe kimaandishi kwenye kitabu cha adhabu.
Kaka wa mwanafunzi huyo Bwana Yasin Sharifu amesema changamoto ya usafiri ndiyo iliyopelekea wao kuchelewa kufika kwa wakati katika shule hiyo, lakini walitoa taarifa kwa Mwalimu Mkuu wa shule na kupata kibali.
Kufuatia maelekezo ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro mwanafunzi huyo amepelekwa Hospaitali ya Rufaa Mkoani hapa ili kubaini kama amepata athari nyingine za kiafya zilizotokana na kipigo hicho.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.