Mhe. Bashungwa aipongeza Menejimenti ya kiwanda cha sukari Mkulazi.
Waziri wa Ujenzi, Mhe. Innocent Bashungwa, ameipongeza Menejimenti ya Kiwanda cha Mkulazi kwa kumpokonya tenda Mkandarasi wa Bouvet Engineering Ltd ya Nchini India kazi ya kuweka barabara kiwango cha lami zinazozunguka kiwanda hicho mara baada ya kushindwa kukamilisha ujenzi huo kwa muda uliopangwa.
Mhe. Bashungwa amesema hayo Februari 22, 2024 alipotembelea ujenzi wa kiwanda na miundombinu ya barabara kwenye Kiwanda cha Sukari Mkulazi kilichopo Halmashauri ya Kilosa.
Mhe. Bashungwa amesema hajaridhishwa na utendaji kazi wa Mkandarasi huyo ambapo amemuagiza Mtendaji Mkuu wa TANROADS kutangaza zabuni ya mradi huo mara moja na kumpata Mkandarasi mwenye sifa na uwezo wa kutekeleza kwa ufanisi mkubwa na kuhakikisha unakamilika ifikapo Aprili mwaka huu.
"..Nipongeze menejimenti Mtendaji Mkuu wa kiwanda cha Sukari Mkulazi kwa hatua mlizochukua ya kumnyang'anya jukumu la ujenzi wa barabara ambazo zinazunguka kiwanda..." Amesema Mhe. Bashungwa.
Bashungwa amesema kukamilika kwa ujenzi wa miundombinu ya kiwanda hicho kilichofikia asilimia 70 kutasaidia kuongeza uzalishaji wa sukari nchini na kupunguza uhaba wa bidhaa hiyo hivyo ameuagiza uongozi wa Kiwanda kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kumsimamia Mkandarasi wa ujenzi wa Kiwanda hicho ili ifikapo mwishoni mwa mwezi aprili 2024 ujenzi wa kiwanda hicho uwe umekamilika kwa asilimia 100.
Aidha Mhe. Bashungwa amemshukuru Rais, Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuweka mazingira wezeshi ya Ujenzi wa viwanda nchini ikiwa ni pamoja na kiwanda cha Sukari cha Mkulazi ambacho kitakuwa na uwezo wa kusaga tani 2500 za miwa na kuzalisha tani 50,000 za sukari kwa mwaka.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Adam Malima, amesema Mkandarasi anayetekeleza ujenzi wa miundombinu ya barabara amekuwa akisua sua na kupelekea shughuli za uzalishaji wa kiwanda hicho kutokufanyika kwa ufanisi, kutokana na ubovu wa miundombinu ya barabara zinazounganisha kiwanda na Mashamba ya miwa, pia magari yanashindwa kuingia mashambani kuchukua miwa na kupeleka kiwandani kwa sababu ya ubovu wa barabara.
Naye, Meneja wa Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) Mkoa wa Morogoro, Mhandisi Alinanuswe Kyamba amesema TANROADS ina jukumu la kusimamia kazi zote za manunuzi, ujenzi wa kiwanda, shughuli zote za ukamilishaji wa kiwanda na kuanza uzalishaji wa sukari katika kiwanda hicho cha Mkulazi na kuleta Manufaa kwa Watanzania.
Mhe.Bashungwa Februari 23, 2024 ataendelea na ziara yake ya kikazi Mkoani Morogoro kwa kutembelea Wilaya Ifakara na Mlimba.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.