Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo Mhe. Deo Mwanyika (MB) amefurahishwa na mpango madhubuti wa utekelezaji wa mazao ya kimkakati Mkoani ili kuhakikisha kuwa sekta ya kilimo inaboresha maisha ya wanamorogoro na watanzania kwa ujumla.
Mhe. Deo Mwanyika amesema hayo Februari 15, Mwaka huu wakati wa ziara ya kamati hiyo Mkoani Morogoro ambapo siku ya kwanza ya ziara hiyo imetembelea Vitalu vya miche ya parachichi na shamba la viazi mviringo katika vijiji vya Mkogwe na Masenge Wilayani Gairo.
Akifafanua zaidi, Mwenyekiti huyo amesema Mkoa huo umefanikiwa kuanzisha mpango wa kilimo cha mazao biashara kama Parachichi, Karafuu, Kokoa, Michikichi na Kahawa ili kuhakikisha wakulima wanazalisha kwa tija na kuinua uchumi wao.
"... Mhe. Rais ameongeza bajeti ya kilimo mara 100 kutoka tsh. Bil. 270 na tunaongelea sasa Trilioni 1.1 na itaongezeka zaidi..." amesema Mhe. Deo Mwanyika.
Aidha, amewahimiza wananchi kupanda miti sambamba na zao la parachichi ili kusaidia kuhifadhi mazingira na kuhakikisha upatikanaji wa mvua ya kutosha kwa kilimo kwani bila miti hali inaweza kusababisha ukame na kurudisha nyuma kilimo hicho.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amesema kuwa Mkoa huo unahakikisha mapinduzi makubwa ya kilimo hasa cha mazao hayo matano na kwa upande wa Wilaya ya Gairo yanaongezeka mazao ya viazi na Tumbaku mkakati unaolenga kuhimili mabadiliko ya tabianchi lakini pia kuondoa dhana ya watanzania walio wengi kuwa kilimo hakina tija.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa, amebainisha kuwa Wilaya ya Gairo hususan sehemu za milimani ina hali ya hewa inayofaa kwa zao la parachichi na viazi mviringo na kwamba wanashirikiana na taasisi mbalimbali kufanikisha mkakati huo ikiwa ni pamoja na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) ambayo imeandaa miche 100,000 ya parachichi na kutoa bure kwa wakulima kwa ajili ya kupanda katika mashamba yao.
Wakati huo huo, Diwani wa Kata ya Chagongwe Mhe. Frank Robert Kyangala ameishukuru Serikali kwa kutoa elimu kwa wakulima ili kuongeza tija ya uzalishaji katika kilimo na kuondoa umaskini katika kata yake huku akiiomba Serikali kuwajengea barabara kwa kiwango cha lami inayotoka Gairo hadi Tarafa ya Nongwe ili kurahisisha usafirishaji wa mazao kwenda sokoni.
Nao wakazi wa Kijiji cha Mkobwe katika Tarafa ya Nongwe akiwemo Bi. Neema Mnjowe ambaye ni mwanachama wa Kikundi cha Mboto kinachojishughulisha na uandaaji wa miche ya parachihi na miti ya mbao amesema wamepata mafunzo ya kuotesha mbegu za parachichi na miti ya mbao ili kumebadilisha maisha yao na kujikimu mahitaji yao muhimu yakiwemo mavazi, malazi na chakula.
Mwisho.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.