Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo Mhe. Deodatus Mwanyika ( Mb) ametoa wito kwa wafanyabiashara kushirikiana na Serikali kwa kutoa taarifa kwa mamlaka husika mara wanapoona watu wenye nia ovu ya kudhoofisha Mfumo huo.
Mhe. Deodatus ametoa wito huo Oktoba 20, 2024 wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo iliyofanyika Wilayani Mvomero Mkoa wa Morogoro yenye lengo la kukagua na kujadili mustakabali wa mazao mbalimbali ya biashara likiwemo zao la Kakao na kusisitiza matumizi ya mfumo wa Stakabadhi Ghalani.
Akifafanua zaidi, Mwenyekiti huyo amesema wafanyabiashara wengi hupata maslahi yao binafsi kwa kutofuata taratibu za manunuzi ya mazao kwa wananchi hivyo amewasisitiza kutoa taarifa ili hatua kali za kisheria zichukuliwe dhidi yao.
".. Mimi nitoe wito tutoe ushirikiano ili tuimarishe huu mfumo, kama tunajua kuna watu wanafanya ujanja ujanja tutoe taarifa kwa wakati kwa viongozi wetu.." amesisitiza Mhe. Deodatus Mwanyika.
Kwa sababu hiyo, Mwenyekiti huyo ameielekeza Bodi ya Stakabadhi za Ghala (WRRB) kueneza mfumo huo katika mikoa yote hapa nchini pamoja na kuongeza idadi ya mazao kutoka kwa wakulima huku akiwataka kufanya kazi kwa bidii na ubunifu ili mfumo huo ufanye kazi kikamilifu na kumnyanyua mkulima.
Sambamba na hayo, Mhe. Mwanyika ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwajali wakulima na kuboresha maisha yao kwa kuwaletea mfumo huo ambao unawasaidia wakulima kuuza mazao yao kwa bei ya elekezi.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Exaud Kigahe (MB) amewataka wakulima kuendelea kujituma, kufanya kazi kwa bidii na kutumia Mfumo wa Stakabadhi za Ghala kwa manufaa yao ili kuinua kipato chao na Taifa kwa ujumla.
Nao wakulima wa Mhonda juu akiwemo Boli Paul Ndege amesema mfumo huo unawasaidia kuweka ile bei elekezi na kuwanufaisha ambapo ni tofauti na hapo awali hakukuwa na ya matumizi ya mfumo huo kwani wakulima walikuwa wakiuza mazao yao kwa bei ya chini.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.