Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na utawala bora Mhe. George Simbachawene (MB) amewataka Waajiri wa watumishi wa umma kutenga bajeti itakayowawezesha watumishi hao kushiriki mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali Tanzania (SHIMIWI) kuanzia hapo mwakani.
Mhe. Simbachawene ametoa agizo hilo Oktoba 5, Mwaka huu Mkoani Morogoro wakati akifunga mashindano ya SHIMIWI yaliyofanyika katika viwanja mbalimbali vya michezo vilivyopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.
Aidha, Waziri huyo amesema kuwepo kwa upungufu wa vilabu kutoka 74 mwaka 2023 hadi vilabu 66 mwaka 2024 ni ishara isiyofaa kwa watumishi wa Umma, hivyo amewataka waajiri watambue umuhimu wa michezo hiyo ili kuanzia mwaka 2025 watumishi wengi washiriki michezo hiyo.
"... nitumie nafasi hii kutoa maelekezo kwa waajiri wote wa watumishi wa umma, kuhakikisha wanatoa fedha za kutosha kwenye mipango na bajeti ili kuwezesha ushiriki wa watumishi katika michezo ya SHIMIWI..." Amesema Mhe. George Simbachawene.
Waziri Simbachawene amesema michezo hiyo inajenga afya ya akili, mwili pamoja na kuepusha magonjwa yasiyo ya kuambukiza kama presha, ugonjwa wa Moyo, mfumo wa upumuaji, mzunguko wa damu, kuimarisha misuli na kuongeza ufanisi wa utendaji kazi wa mwili.
Aidha, Mhe. Simbachawene ametumia fursa hiyo kuwataka watumishi hao wa umma kwa upande wao kufanya kazi kwa bidii katika maeneo yao ya kazi kwa kutoa huduma bora kwa wananchi
Akiongea kuhusu uchaguzi, Waziri huyo amewaagiza Makatibu Wakuu, Makatibu Tawala wa Mikoa na Wakuu wa Sehemu na Vitengo kuhakikisha wanajiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura ili kushiriki uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika Novemba 27, Mwaka huu kwani amesema watumishi hao wamekuwa na kasumba ya kutoshiriki chaguzi hizo.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amesema Mkoa huo unasifika kwa michezo kutokana na Amani iliyopo ambayo ndio chachu ya maendeleo na kuwashukuru wanamichezo wa SHIMIWI kwa kufanya utalii wa kutembelea Mbuga za Mikumi, hifadhi ya Mwalimu Nyerere na Udzungwa pamoja na vivutio vingine vilivyopo ndani ya Mkoa huo.
Mwenyekiti wa SHIMIWI Taifa Bw. Daniel Mwalusamba ameishukuru Wizara ya Utamaduni, Sanaa, na Michezo kwa kutoa miongozo iliyosaidia kufanikisha usimamizi wa michezo hiyo na kwamba pamoja na jukumu hilo bado wameshiriki kwenye masuala kijamii ambapo wametembelea vituo vya kulea watoto yatima ndani ya Manispaa ya Morogoro na kutoa vifaa mbalimbali kulingana na uhitaji.
Michezo hiyo ya 38 tangu kuanzishwa kwake imejumuisha wanamichezo 20995 ambapo wanaume ni 1683 na wanawake ni 1312 kutoka katika Wizara 20, Mikoa 19, Wakala wa Serikali 3 na Taasisi za Umma 14.
Mwisho
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.