Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Fatma Mwassa amesema kwa kutambua kuwa lishe bora ni kichocheo katika Nyanja zote za maendeleo, Serikali imeazimia kufanya tathmini ya kila mwaka kuhusu hali ya lishe na tathmini maalum ya kila baada ya miaka mitano kwa lengo la kuhakikisha kuwa taifa linakuwa na wananchi wenye afya bora na wenye uwezo wa kuchangia shughuli za maendeleo.
Fatma Mwassa amesema hayo Agosti 5, 2022 mwaka huu wakati wa kikao cha tathmini ya nusu Mwaka cha Lishe ngazi ya Mkoa kilichofanyika katika Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo ikiwa ni kikao chake cha kwanza kujadili masuala ya lishe tangu ateuliwe kuongoza Mkoa huo.
Akifafanua zaidi Mkuu huyo wa Mkoa amesema ili Mkoa uweze kukabiliana na utapiamlo inatakiwa mikakati na mipango thabiti yenye lengo la kuwekeza katika lishe na kuhakikisha shilingi 1000 ambazo Halmashauri zilielekezwa kutenga kutoka katika vyanzo vyao vya mapato kwa ajili ya kuboresha lishe kwa watoto chini ya umri wa miaka mitano zinatengwa na kutumika kwa nia hiyo.
Kwa upande wake Afisa Lishe wa Mkoa wa Morogoro Salma Magembe amesema Mkoa bado unakabiliwa na tatizo la udumavu kwa kiasi kikubwa, kwani pamoja na takwimu kuonesha tatizo hilo linapungua kutoka asilimia 33.4 2015/2016 hadi asilimia 26.4 mwaka 2018 bado Mkoa huo una idadi watoto laki moja mia saba na thelathini wenye udumavu.
Hata hivyo Bi.Salma amesema Mkoa umejipanga kutatua changamoto hiyo kwa kutoa Elimu kuhusu utumiaji wa vyakula kwa watoto huku akibainisha kuwa Mkoa wa Morogoro una vyakula vingi vya aina tofauti tatizo ni Elimu ya namna ya kupangilia kutumia vyakula hivyo eneo ambalo amesema linatakiwa kuwekewa mkazo zaidi kupitia watendaji wa Serikali wa ngazi mbalimbali.
Mkuu wa Wilaya ya Malinyi Mkoani Humo Mathayo Masele yeye anatoa wito kwa watendaji wote wa Serikali zikiwemo Ofisi za Wakuu wa Wilaya kuendelea kushirikiana na Ofisi za Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri katika kuhamasisha wananchi ili kuondokana na suala la utapiamlo na udumavu kwa watoto.
Nao washiriki wa kikao hicho akiwemo Afisa Lishe wa Halmashauri ya Mlimba Simoni Mkali amewataka wananchi kuondokana na mila potofu zinazochangia udumavu kwa watoto, ikiwemo ya kumwaga maziwa ya mama anayoyatoa saa moja baada ya kujifungua kwa kuamini kuwa ni maziwa hayo ni machafu jambo ambalo sio sahihi.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.