Wadau wa maendeleo Mkoani Morogoro wamesifu hatua za maendeleo ambayo nchi ya Tanzania imefikia ukilinganisha na hali ya nchi hiyo wakati inapata uhuru ambapo nchi ilikuwa katika hali isiyoridhisha kimaendeleo.
Sifa hizo zimetolewa Disemba 9 mwaka huu na wadau mbalimbali kwenye Mdahalo wa kujadili maendeleo endelevu ambayo Halmashsuri ya Manispaa ya Morogoro imefikia katika kipindi cha miaka 61 ya Uhuru wa Tanzania, mdahalo huo umefanyika kwenye ukumbi wa mikutano uliopo Manispaa ya Morogoro.
Miongoni mwa wadau hao ni Bw. Deograsias Mhaiki ambaye ni Afisa Elimu Taaluma Manispaa ya Morogoro amesifu maendeleo yaliyopatikana katika sekta ya elimu ambapo hapo awali shule zilikuwa chache na nafasi ya wanafunzi kuchaguliwa kujiunga na shule za sekondari ilikuwa ni nadra sana.
Aidha, ameongeza kuwa kwa sasa katika Manispaa hiyo wanafunzi wanapata nafasi ya kujiunga na elimu ya sekondari kwa kuwa shule ni nyingi takribani 29, hata changamoto ya vyumba vya madarasa kwa sasa imepungua, pia hakuna chaguzi tatu kama ilivyokuwa hapo awali.
Kwa upande wake Bw. Jeremiah Lubeleje Mchumi wa Manispaa ya Morogoro amepongeza juhudi kubwa iliyofanyika katika kuboresha miundombinu hapa nchini na amesema watanzania wanasababu ya kujivunia katika hilo kwa sababu kuna baadhi ya nchi kama vile msumbiji wananchi wake waishio mipakani wamekuwa wakifuata huduma za afya nchini Tanzania.
Sambamba na hilo Mchumi huyo amewashauri vijana ambao wamehitimu elimu ya sekondari na vyuo vikuu hapa nchini kutokubweteka badala yake wajishughulishe na shughuli mbalimbali ikwemo kilimo au ufugaji kwa lengo la kujikwamua kutokana na changamoto ya ajira.
Bi. Amina Rashid mwandishi wa habari kutoka kituo cha Planet Redio amesema kuna mabadiliko makubwa katika teknolojia ya habari na mawasiliano ambapo kwa sasa watu wanapata taarifa na matukio kutoka maeneo mbalimbali hapa duniani kupitia simu zao za viganjani, tofauti na hapo awali wakati nchi inapata uhuru redio, televisheni na simu zilikuwa chache hivyo taarifa zilikuwa zinachelewa kuwafikia watu.
Nae Bw. Bakari Nsulwa ambaye alikuwa mwenyekiti wa mdahalo huo wakati akihitimisha majadiliano amesema watanzania wanatakiwa kuendelea kudumisha Amani, umoja, na mshikamano tulionao kwani ndiyo silaha pekee katika mustakabali wa maendeleo ya Taifa letu.
Aidha mwenyekiti huyo amesisitiza watanzania kuwa wazalendo na nchi yao kwani hata mataifa makubwa yameimarika kutokana na wananchi wake kuwa wazalendo kwa nchi zao.
Kwa upande wake Bw. Silas Ikanga ambaye ni Mhasibu wa Taasisi ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Mkoani Morogoro amesema watanzania wanapaswa kumuenzi Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius kambarage Nyerere kwa kupinga ukabila, udini, pamoja na ukanda, hata hivyo amesisitiza wanamorogoro kuishi maono na fikra za Mwalimu Nyerere.
Uhuru wa Tanganyika ulipatikana mnamo Disemba 9 mwaka 1961, kutoka kwa waingereza na Mwalimu J. K. Nyerere alikuwa Waziri Mkuu wa kwanza.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.