Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amesema michezo ni moja ya nyenzo muhimu hapa nchini katika kupambana na uharifu na matumizi ya madawa ya kulevya.
Makamu wa Pili wa Rais amesema hayo Septemba 6, 2024 Mkoani Morogoro wakati akizindua mashindano ya Michezo ya Majeshi hapa nchini yaliyoratibiwa na Baraza la Michezo ya Majeshi ya Tanzania (BAMMATA) na kufanyika katika uwanja wa Jamhuri uliopo Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro yakiwa na lengo la kukuza na kuendeleza vipaji vya vijana.
Mhe. Hemed Suleiman amesema, michezo inasaidia katika kupambana na kuzuia uharifu na matumizi ya madawa ya kulevya ndani ya jamii kwa njia ya kuwashawishi wananchi hususan vijana kujiunga kwenye michezo ili kuepusha kujiingiza kwenye vitendo viovu hususan ubakaji, wizi, ujambazi na matendo mengine yasiyokubalika katika jamii.
"...mara kadhaa tumekuwa tukitumia michezo kama nyenzo ya kupambana na uharifu na matumizi ya madawa ya kulevya kwa kuwashawishi vijana kujiunga kwenye michezo..." amesema Mhe. Hemed Suleiman
Aidha, Makamu huyo wa Pili wa Rais wa Zanzibar amesema, michezo inajenga afya ya akili, mwili pamoja na kuepusha magonjwa mbalimbali yakiwemo presha, Moyo na mfumo wa upumuaji ndani ya majeshi na kwa wananchi kwa ujumla.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa BAMMATA Brigedia Jeneral Said Hamisi Said amesema mashindano hayo yatafanyika kwa siku 10 kuanzia Septemba 6 hadi 15, 2024 na kutaja michezo itakayochezwa katika mashindano hayo kuwa ni mpira wa Miguu, mpira wa mikono, mpira wa kikapu, mpira wa wavu, mchezo wa riadha, mchezo wa ngumi, mchezo wa vishale na kulenga shabaha
Sambamba na hayo amebainisha Viwanja vitakavyotumika kwenye mashindano hayo ndani ya Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro kuwa ni viwanja vya Jamhuri, viwanja vya Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine - SUA, viwanja vya chuo cha Kijeshi cha Pangawe na viwanja vya Bwalo.
Mwisho.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.