.
Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imerejesha Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali – SHIMIWI iliyokuwa imesimamishwa tangu mwaka 2015.
Hayo yamebainishwa Oktoba 19 mwaka huu na Mwenyekiti wa SHIMIWI Taifa Daniel Zacharia alipokuwa anazungumza na waandishi wa habari katika uwanja wa Jamhuri uliopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro wakati wa maandalizi ya mashindano hayo.
Zacharia amebainisha sababu ya kusimamishwa kwa michezo hiyo kwa kipindi hicho cha miaka mitano kuwa inatokana na Serikali kuelekeza fedha iliyokuwa inatumika katika michezo hiyo kwenye shughuli za wa miradi ya maendeleo iliyokuwa ikitekelezwa wakati huo.
Katika hatua nyingine, Zacharia amebainisha lengo la mashindano ya SHIMIWI kwa watumishi wa Umma kuwa ni kuwajengea fursa wafanyakazi hao kufahamiana, kushirikiana, kujenga udugu na mazoea ili kurahisisha utendaji mzuri katika sehemu zao za kazi.
Aidha, amesema katika kipindi ambacho michezo hiyo ilisimama, Serikali ilielekeza watumishi wote wa Serikali kufanya mazoezi katika kila wiki ya kwanza ya mwezi ili kujenga Afya zao vizuri hususan kipindi hiki ambacho dunia nzima inakabiliwa na ugonjwa wa UVIKO – 19.
‘’Watumishi wetu kama watakuwa na Afya njema watashiriki kikamilifu katika shughuli za ujenzi wa taifa, kwa hiyo tunaishukuru Serikali na uongozi mzima wa taifa hili’’ amesema Zacharia.
Awali akizungumza na waandishi wa habari Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela amesema uzinduzi rasmi wa mashindano hayo ya SHIMIWI unatarajiwa kufanyika Oktoba 23 mwaka huu katika uwanja wa Jamhuri Mjini Morogoro na mgeni Rasmi katika uzinduzi huo atakuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Isdor Mpango.
Shigela amesema michezo mbalimbali inayotarajiwa kufanyika katika mashindano hayo ni pamoja na mpira wa miguu, kuvuta kamba, kukimbiza kuku, mpira wa pete, netball, mashindano ya kukimbia na michezo mingine.
Sambamba na hayo, Shigela ametumia fursa hiyo kuwakaribisha wananchi wote wa Mkoa wa Morogoro kushiriki na kushuhudia mashindano ya michezo hiyo na kuwataka wananchi wa Mkoa huo kutoa ushirikiano, kuwaonesha upendo, kuwasaidia ili viongozi wake waweze kuvutiwa na ikiwapendeza mashindano yajayo tena yaweze kufanyika Mkoani humo.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.