Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Mussa Ali Mussa amesema kuwepo kwa sayansi na teknolojia kumesaidia utendaji kazi kuwa wa kasi na wa haraka hapa nchini ambapo amewataka wakaguzi wa Halmashauri za Mkoa huo kutumia mifumo ya GOTHOMIS, FFARS na NeSTi ili kuboresha utendaji kazi kuwa wa wazi na kuondoa udanganyifu wa watumishi wa umma.
Dkt. Mussa amesema hayo Novemba 11, Mwaka huu wakati akifungua mafunzo ya mifumo ya GOTHOMIS Centralized, FFARS na NeST kwa Wakaguzi wa Halmashauri za Mkoa wa Morogoro yanayowezeshwa na Wakufunzi kutoka Ofisi Rais TAMISEMI na kutoka Mamlaka ya ununuzi wa Umma (PPRA).
Mafunzo hayo yaliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro yamelenga kuwajenga uwezo Wakaguzi wa ndani kuhusu ukaguzi wa shughuli mbalimbali zinazotekelezwa katika mifumo hiyo.
Aidha, Katibu Tawala huyo wa Mkoa amewataka wakaguzi hao kufuatilia kwa kina mafunzo hayo ili kuwa na uelewa katika matumizi yake kwa ajili ya kufanya ukaguzi wa shughuli zinazotekelezwa na kuongeza ufanisi katika utendaji kazi kwani amesema maendeleo ya sayansi na teknolojia yanalenga kuongeza uwazi na uwajibikaji kwa watumishi wa umma hususan ndani ya Halmashauri za mkoa wa Morogoro.
Kwa upande wake, Mganga mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Best Magoma amesema mafunzo hayo yamelenga kutoa uelewa wa pamoja kwa wakaguzi wa halmashauri katika kutekeleza majukumu yao na kuongeza kuwa mifumo hiyo inazisaidia sekta za afya hususan katika ukusanyaji wa mapato ya vituo vya afya ili kuweza kujiendesha vyenyewe.
Pia amesema watumishi wa umma wanapaswa kuendana na kasi ya teknolojia kuhama kutoka mifumo ya “analogy” kwenda mifumo ya “Digital” ikiwemo matumizi ya mifumo hiyo ya GOTHOMIS, FFARS na NeST yote ina lengo la kurahisisha utekelezaji wa majukumu.
Mwisho.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.