Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Mhandisi Emmanuel Kalobelo amebainisha kuwa migogoro ya Ardhi katika Mkoa huo imepungua kwa kiasi kikubwa kutokana na Serikali ngazi ya Taifa, Mkoa pamoja na Wilaya kwenda kutatua migogoro hiyo moja kwa moja kwenye maeneo husika.
Mhandisi Kalobelo amebainisha hayo hivi karibuni Ofisini kwake alipokuwa anaongea na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Angelina Mabula alipofanya ziara ya kikazi ya siku moja Mkoani humo.
Amesema Migogoro iliyobaki sasa ni ile ya Wananchi wachache kuwa na tabia ya kuvamia hifadhi za Taifa na sio migogoro baina ya mtu na mtu au baina ya jamii ya wakulima na wafugaji ambayo ilisumbua sana miaka ya nyuma.
Amebainisha kuwa sababu kubwa ya kupungua kwa migogoro hiyo ni pamoja na baadhi ya Wilaya kupitiwa na Mradi wa urasimishaji wa Ardhi uliojulikana kama Land Tenure support Programme katika Wilaya za Ulanga, Malinyi na Kilombero ambapo vipande vyote vya ardhi vya Wilaya hizo vilirasimishwa hivyo kupunguza migogoro ya Ardhi.
Sababu nyingine ni Viongozi wa Serikali katika ngazi zote kutumia muda mwingi kwenda kutatua kero hizo kwenye tukio badala ya kutatua migogoro hiyo kuwa Ofisini jambo ambalo pia limesaidia kupata ukweli zaidi na kuondoa pengine kutatua migogoro pasipo kuona ukweli na uhalisia.
“Mkoa wa Morogoro ulionekana kama ni Mkoa wa Migogoro ya Ardhi, lakini kwa Ushirikiano na Wizara yako nipende kusema migogoro imepungua sana kutokana na hatua mbalimbali ambazo zimekuwa zikichukuliwa” alisema Mhandisi Kalobelo.
Aidha, ameongeza kuwa uamuzi wa Serikali wa kuwabadilishia vituo vya kazi Maafisa wa Ardhi wa Mkoa wa Morogoro kwa wakati mmoja na kuwaleta Maafisa wengine wapya umechangia kupunguza kero kwa kuwa zoezi hilo liliongeza uwajibikaji kwa maafisa Ardhi hao wapya kwa kutekeleza majukumu yao ya kikazi kikamilifu (commitment).
Kuhusu wananchi kuendelea kuvamia hifadhi, Kalobelo amesema tayari Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Loata Ole Sanare amekwisha litolea maelekezo suala hilo kuhakikisha maeneo yote ya hifadhi Mkoani humo yanalindwa kwa mujibu wa sheria zilizopo.
Kwa upande wake Naibu Waziri Angelina Mabula pamoja na kupongeza hatua za Mkoa kupunguza migogoro ya Ardhi amesema ni muhimu Elimu iendelee kutolewa kwa wananchi waliorasimishiwa ardhi zao na kupewa hati miliki za kimila kwa ajili kuendeleza uchumi wa familia zao kwa kuzitumia hati hizo kupata mikopo katika taasisi za kibenki kwa kuwa zinatambulika.
Aidha, amesema Wilaya ambazo zina mashamba pori yaliyofutiwa umiliki wake, zitatakiwa kufanya maandalizi ya matumizi ya mashamba hayo mara Mkoa utakapopokea maelekezo ya Serikali, Wilaya hizo zinatakiwa kujipanga na kuwa na Mpango wa matumizi sahihi ya mashamba hayo ambayo Serikali itawajulisha muda mchache ujao.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.