Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amesema miradi ya maendeleo ikiwemo madaraja, barabara, viwanda, shule na hospitali inayotekelezwa na Serikali Mkoani Morogoro inalenga kutatua changamoto za msingi zinazowakumba wananchi katika maeneo yao sambamba na kubadilisha maisha yao.
Mhe. Adam Malima amesema hayo Oktoba 11, 2023 alipokuwa anaongea na wanafunzi wa Chuo cha Ukamanda na Unadhimu (CSC) cha Duluti Mkoani Arusha waliofika Mkoani hapa Oktoba 9 kwa ziara ya siku tano kwa lengo la kujifunza mambo mbalimbali ya kimaendeleo.
"... maendeleo maana yake ni misingi ya kubadilisha maisha ya wananchi wanaopelekewa miradi hii, kama Mkoa wa Morogoro fedha zinazokuja tunahakikisha zinaenda kutatua matatizo yanayohusiana na maendeleo kwa wananchi..."
Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa amesema Serikali haijengi miundombinu hiyo kwa kujifurahisha bali kulingana na mahitaji na umuhimu wa miradi husika katika eneo hilo kwa sababu fedha zinazotumika ni za wananchi, hivyo wajibu wa Serikali ni kutekeleza miradi itakayowanufaisha wananchi wa eneo husika.
Sambamba na hayo, Mkuu huyo wa Mkoa amesema Mkoa wa Morogoro ni mzalishaji Mkuu wa zao la karafuu hapa nchini baada ya Visiwa vya Pemba ambalo linauzwa kilo moja Tsh. 18,000 huku akibainisha mazao mengine ya biashara yanayoweza kustawishwa mkoani humo kuwa ni pamoja na tangawizi, Kakao na pilipili mtama hivyo kuwataka wakulima Mkoani humo kulima mazao hayo ili kuongeza kipato chao naTaifa.
Katika hatua nyingine Mhe. Adam Kighoma Ali Malima amewataka wafugaji mkoani humo kubadili mtindo wao wa kufuga, kuwa na mifugo michache na yenye tija badala ya kuwa na mifugo mingi isio na tija kwao na kusababisha migogoro baina yao na wakulima.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.