Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Mussa Ali Mussa amewataka wadau wanaotekeleza miradi ya kuwainua Vijana kiuchumi Mkoani humo wajikite katika utunzaji wa mazingira ili kurudisha uoto wa asili.
Dkt. Mussa ametoa kauli hiyo Machi 5, 2024 wakati wa kikao kifupi na wadau wanaotekeleza mradi wa kuwainua vijana kiuchumi Mkoani humo, kikao hicho kimefanyika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo.
Katibu Tawala huyo amepongeza jitihada za wadau hao katika kutatua changamoto za kiuchumi kwa vijana kupitia kilimo cha mazao ya viungo ikiwemo michaichai, karafuu, mdarasini na vanila huku akitaka miradi hiyo iambatane na utunzaji wa mazingira, kwani kwa kufanya hivyo itasaidia kurudisha uoto wa asili kama Mkoa wa Morogoro ulivyokuwa awali.
“...hivi viungo kama vitapandwa kikweli kweli vitatunza mazingira ya huku juu...” amesema Dkt. Mussa.
Aidha, Dkt. Mussa amewataka vijana ambao wamepatiwa miradi ya kilimo cha mazao ya viungo kujikita katika uongezaji wa thamani wa mazao hayo.
Naye Mratibu wa mradi huo amemshukuru Katibu Tawala huyo na kuahidi kuyafanyia kazi maelekezo aliyoyatoa wakati wa kikao hicho kuboresha miradi yao hivyo kuwasaidia vijana hao kujikwamua kiuchumi.
MWISHO.
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.