MKAKATI WA LISHE BORA NI SEHEMU YA MALENGO YA SERIKALI KUELEKEA KWENYE MAPINDUZI YA VIWANDA
Mkuu wa Mkoa wa Pwani Aboubakar Kunenge ambaye pia ni Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Morogoro amesema mkakati wa lishe bora hapa nchini ni moja ya malengo ya Serikali kuelekea kwenye mapinduzi ya viwanda na maendeleo ya nchi kwa kuwa ubora wa mtu kiakili katika kuleta mapinduzi unategemea siku 1000 tangu mama kutungwa mimba.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani Aboubakar Kunenge wakati aikifungua Mkutano wa Tathmini ya Mkataba wa Lishe na Bima ya Afya Mkoani Morogoro, Febr. 15 mwaka huu
Aboubakar kunenge amesema hayo Februari 15 mwaka huu wakati akifungua mkutano wa nusu mwaka wa tathmini ya Mkataba wa lishe na Bima ya Afya ya Jamii iCHF uliofanyika katika Ukumbi wa mikutano wa CCT uliopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.
RC Kunenge akiwana mwenyeji wake Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Mariam Mtunguja kwenye kikao cha tathmini ya Mkataba wa Lishe na Bima ya Afya ya iCHF Mkoani Morogoro, Februari, 15 mwaka huu
Aboubakar Kunenge ambaye kwa sasa ni kaimu Mkuu wa Mkoa wa Morogoro amesema, ili nchi iweze kupata maendeleo na kusonga mbele ni muhimu kutilia mkazo suala la Lishe Bora hususan malezi ya mtoto ndani ya siku 1000 tangu mama kutungwa mimba kipindi ambacho hupelekea ubora unaohitajika kwa mtoto atakayezaliwa na hivyo kuweza kuleta maendeleo katika nchi.
“Kwa hiyo lazima tuhakikishe mkakati wa kuinyanyua nchi yetu…. ni aina ya watu kwa sababu ‘what matters most’ katika resources za aina yoyote tulizo nazo ni Rasilimali Watu. Na ubora wa Rasilimali Watu kwa mujibu wa Sayansi ni siku 1000 za kwanza” amesema RC Kunenge.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani Aboubakar Kunenge akiteta jambo na Mkuu wa Wilaya mwenyeji wilaya ya Morogoro Albert Msando (kushoto)
Kwa sababu hiyo, Mhe. Kunenge amewataka viongozi wa Mkoa wa Morogoro na watumishi wote wa umma kutekeleza mkataba wa Lishe huku akiwataka Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri kutosa fedha zinazohitajika kutekeleza mkataba huo bila kusukumwa na mtu kwa kuwa kila mtendaji atapimwa utendaji wake kutokana na namna alivyotekeleza Mkataba huo.
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Mkoa amewataka viongozi na watumishi wote wa Serikali Mkoani humo kusimamia kwa dhati zoezi la Anwani za Makazi, huku akibainisha kuwa zoezi hilo lina umuhimu kwa zoezi la Sensa ya watu na Makazi linalotarajiwa kufanyika mwezi Agosti mwaka huu.
Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro Mhe. Pascal Kihanga akiwa katika kikao cha tathmini ya Lishe kilichoongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Amesema zoezi la Sensa ya Watu na Makazi sio geni hapa nchini, limekuwa likifanyika kila baada ya miaka kumi, hata hivyo zoezi hilo kimsingi limekuwa linafanyika upande mmoja wa Sensa ya watu pekee huku suala la makazi likiachwa na kwamba mwaka huu itakuwa ni mara ya kwanza zoezi la Makazi kufanyika, hivyo ufanisi wa Sensa ya watu ya mwaka huu inategemea sana utekelezaji wa zoezi la anwani za Makazi ambalo linatakiwa kukamilika kabla au ifikapo mwezi Mei mwaka huu.
Baadhi ya Wakuu wa Wilaya walioshiriki kikao hicho. Juu ni Ngollo Malenya Mkuu wa Wilaya ya Ulanga na chini ni Hanji Godogodi Mkuu wa Wilaya ya Kilombero
Kwa sababu hiyo, amewakumbusha watendaji kutekeleza zoezi la anwani za Makazi kwa mujibu wa maelekezo ya Mhe. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwa ni pamoja na kwanza kulifanya zoezi hilo kama operesheni, pili Wakurugenzi kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa zoezi hilo lakini pia kuwa waadilifu dhidi ya fedha za zoezi hilo na kamwe fedha hizo zisitumike kama posho.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Kusirye Ukio akiwa katika kikao cha Tathmini
Akizungumzia zoezi la chanjo ya UVIKO – 19, Mkuu wa Mkoa Aboubakar Kunenge ameagiza kila mmoja kujiwekea mikakati ya kuhamasisha zoezi la chanjo kwa lengo la kuokoa maisha ya watanzania wengine, huku akibainisha kuwa itakuwa aibu na fedhea kubwa kwa Tanzania endapo dawa hizo za chanjo zitaharibika (expire) wakati watanzania wako katika changamoto ya kupoteza maisha kutokana na ugonjwa ambao dawa zake zinaharibika.
Baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa na Wilaya walishiriki kikao hicho.
Kwa upande wake Mratibu wa huduma za chanjo Mkoa wa Morogoro Dkt. Masumbuko Igembya amesema walengwa wa chanjo ya UVIKO – 19 Mkoa wa Morogoro hiyo ni 1,759,666 na waliochanja hadi Februari 15, 2022 ni watu 150,326 pekee sawa na 9% tu ya wakazi wa Mkoa wa Morogoro ukilinganisha na lengo la 60% la wakazi hao ambao wana sifa ya kuchanjwa.
Hata hivyo, amesema idadi ya wagonjwa wenye maambukizi ya ugonjwa wa UVIKO – 19 katika Mkoa huo imepungua na wagonjwa ambao wanafika katika vituo vya kutolea huduma za afya na kugundulika kuwa na ugonjwa huo hususan wanaofikia hatua ya kulazwa na kuwa na hali mbaya ni wale ambao hawajapata chonjo ya UVIKO -19.
Hata hivyo Dkt. Masumbuko amesema changamoto kubwa inayowakabili katika zoezi la chanjo ni idadi ndogo ya watu wanaostahili kupata chanjo mara ya pili kushindwa kumalizia dozi ya pili, huku akibainisha kuwa hadi sasa wlengwa 20,000 ambao wamestahili kupanta chanjo mara ya pili wameshindwa kurudi na kumalizia dozi ya pili. Amesema hali hiyo inaashiria kwamba wateja hao hawana kinga kamili ya UVIKO 19 na kutoa wito kwao kurudi kukamilisha dozi hiyo ili kujihakikishia kinga kamili ya ugonjwa huo.
Naye mratibu wa iCHF Mkoa wa Morogoro Elisia Mtesigwa amesema lengo la Mkoa huo kwa mwaka 2021/2022 ilikuwa kuandikisha kaya 50,600 katika bima hiyo lakini hadi kufikia Februari 15, mwaka huu walikuwa wameandikisha kaya 8,900 pekee jambo ambalo amekiri kuwa bado kuna kazi kubwa ya kufanya.
Mratibu wa Bima ya iCHF Mkoa wa Morogoro Bi. Elisia Mtesigwa akiwasilisha taarifa ya tathmini ya Bima hiyo mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani Aboubakar Kunenge ambaye anakaimu nafasi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro
Baadhi ya Halmashauri zilionekana kufanya vizuri katika baadhi ya maeneo ya utekelezaji wa Mkataba huo na hivyo kupongezwa.
Hata hivyo Mtesigwa ameendelea kuwahamasisha wananchi kujiunga na mfuko wa Bima ya Afya ya iCHF kwa kuwa una gharama ndogo ya matibabu ambapo mchango wa shilingi 30,000/= unaotolewa na mwanachama una uwezo wa kutoa matibabu kwa watu sita kwa mwaka mzima tena mahali popote atakapokuwepo ndani ya Tanzania.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.