Mkandarasi anayejenga Ofisi mpya ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mbeya University of Science and Technology, MCB CO. Ltd, ametakiwa kuongeza kasi ya utendaji wake wa kazi na kuhakikisha anakamilisha kazi hiyo kabla au ifikapo mwezi Mei Mwaka huu.
Hayo yamebainika Februari 26, Mwaka huu wakati wa kikao (Site meeting) kilichoitishwa kwa ajili ya kuangalia maendeleo ya ujenzi wa jengo hilo jipya ambacho kimefanyika eneo la mradi ambao upo mkabala na Ofisi za sasa za Mkuu huyo wa Mkoa.
Wajumbe wa kikao hicho walimtaka Mkandarasi huyo kuongeza kasi ya kukamilisha ujenzi wa jengo hilo kwa kutumia njia nyingine ikiwemo ya kumtafuta mzabuni wa kuleta vifaa vya ujenzi vya kutosha kwa utaratibu utakaokubalika pande zote, kuongeza mafundi wa ujenzi na wafanyakazi lengo ni lile lile la kukamilisha mradi huo kabla ya mwezi Mei, 2025.
Kwa upande wake Mkandarasi wa kazi hiyo Mbeya University of Science and Technology, MCB CO. Ltd, pamoja na kupokea agizo hilo, amemuomba Mshauri mwelekezi wa mradi (Consultant) na mtumiaji wa jengo (Client) kila mmoja kwa nafasi yake kufanya kila wanaloweza kumlipa kwa wakati malipo ya kazi yake kila anapoomba kulipwa kwa mujibu wa Mkataba ili kutekeleza agizo hilo.
Mradi huo wa ujenzi wa jengo la Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro ulianza kujengwa Mwezi Mei, 2022 na kwa mujibu wa mkataba uliopo, mradi huo wa ujenzi ulitarajiwa kukamilika tarehe 26/05/2024 ambapo muda wake umepita zaidi ya miezi Nane na ujenzi uko asilimia 60%.
Fedha za Ujenzi wa Ofisi mpya ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro zimetolewa na Serikali Kuu ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambalo hadi kukamilika kwake litagharimu zaidi ya shilingi za kitanzania Bil. 6.5, huku Mshauri mwelekezi wa kazi hii akiwa ni Tanzania Buildings Agency (TBA)
Kikao hicho kilishirikisha pande tatu zinazohusika na mradi huo ambazo ni Mkandarasi anayejenga jengo (Contractor), Mshauri mwelekezi wa mradi huo (Consultant) na mtumiaji wa jengo hilo (User/Client) kwa maana ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.