Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Morogoro Mhandisi Joseph Masunga amewaagiza Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Malinyi kukamilisha ujenzi wa mradi wa maji wa kata ya Igawa ifikapo oktoba 30 mwaka huu.
Mhandisi Masunga ametoa agiza hilo septemba 28, mwaka huu wakati wa ziara ya wajumbe wa kamati ya siasa ya Mkoa huo kutembelea baadhi ya miradi ya maendeleo inayotekelezwa ndani ya Mkoa leo wakiwa Wilayani Malinyi ili kujionea hatua ya miradi ilipofikia na ubora wake.
Akitoa agizo hilo, Mwenyekiti huyo amesema mradi huo wenye thamani ya Tsh. Milioni 855 ulipaswa kukamilika Julai 7, 2022 hivyo, amewataka watendaji wa RUWASA kukamilisha mradi huo haraka ili kutatua kero ya upatikanaji wa maji kwa wakazi 18674 waliopo katika vijiji vitatu vya Igawa, Lugala na Kiwale.
"… unatakiwa ukamilishe mradi kwa wakati kama ulivyoahidi hapa, wananchi waanze kupata maji katika kata ya Igawa…" amesema Mhandisi Joseph Masunga.
Katika hatua nyingine, Mhandisi Joseph Masunga amewataka wahandisi wa ujenzi wa barabara ya Itete Njiwa hadi Ipera itakayogharimu Tsh. Mil. 266 kukamilisha mradi huo kwa wakati huku akimtaka msimamizi wa mradi huo uliofikia 65% amlipe kwa wakati mkandarasi ili aweze kutekeleza vema mkataba wake na maagizo anayopewa.
Sambambana hayo, Mwenyekiti Masunga ameipongeza serikali ya awamu ya sita ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji thabiti katika sekta ya elimu ukiwemo ujenzi wa shule ya msingi wa Misegese na kuwapongeza wasimamizi wa mradi huo kwa kusimamia maono ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Kwa upande wake, Meneja wa RUWASA Wilaya ya Malinyi Mhandisi Marco Chogero amebainisha kazi zinazoendelea kufanyika ni ujenzi wa fensi eneo la tanki, uchimbaji na ulazaji wa mabomba na ujenzi wa vituo vya kuchota maji huku akiahidi kazi hizo zote kukamilika kabla au ifikapo Oktoba 30, 2024 kama ilivyoagizwa.
Naye Diwani wa Kata ya Igawa Mhe. Sevalius Kamguna amesema amefurahishwa na ujio wa kamati ya siasa wilayani humo kwani amesema inaongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo kupitia maelekezo yanayotolewa na Kamati hiyo.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.