Wilaya za Mkoa wa Morogoro kupitia Halmashauri zake zimetakiwa kufahamu na kujiwekea malengo yakilimo kwa msimu wa kilimo wa mwaka 2020/2021 katika kuzalisha mazao ya Biashara na ya chakula ili mwisho wa msimu huo zifanye tathmini kujua kama Wilaya na Mkoa kwa ujumlaunasonga mbele kwa upande wa sektahiyo ya Kilimo ama unarudi nyuma.
Maagizo hayo yametolewa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Mhandisi Emmanuel Kalobelo Novemba 26 mwaka huu wakati wa maadhimisho ya uzinduzi wa Msimu wa Kilimo 2020/2021 yaliyofanyika Kimkoa katika Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba Wilayani Kilombero Mkoani humo.
Mhandisi Kalobelo alikuwa mgeni rasmi katika maadhimisho hayo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huo Loata Ole Sanare,amesemaMkoa wa Morogoro ni Mkoa wa Kilimo na ni Ghala la chakula la Taifa, hivyo kuna kila sababu ya kuchukua hatua za makusudi katika kuendeleza Sekta ya kilimo ili heshima ya Morogoro kuwa ghala la chakula iwe na maana.
Mhandisi Kalobelo amesema, lengo la agizo hilo ni kutaka kujua malengo waliyojiwekea kwa kila Wilaya kama yametekelezwa au ayakutekelezwa na sababu zilizopelekea kutotekelezwa malengo hayo hatua ambayo itasaidia kujua mwelekeo wa sekta ya kilimo ndani ya Mkoa.
“hakikisheni kila Wilaya inafahamu malengo yake ya msimu wa mwaka 2021 kwa upande wa mazao ya chakula na mazao ya biashara ….kwa sababu ya kufanya hivyo ni kutaka kujua kama tunakwenda mbele au tunarudi nyuma”alisema Mhandisi Kalobelo.
Sambamba na maagizo hayo, Mhandisi Kalobelo amewataka Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri za Mkoa huo kuhakikisha wanaweka utaratibu mzuri wa kutoza ushuru wa mazao ya kilimo kwa wakulima au wafanyabiashara wanaosafirisha mazao hayo kwa lengo la kuepuka kuwatoza ushuru huo zaidi ya mara moja na kwamba hilo litafanikiwa endapo wataimarisha mawasiliano kwa Halmashauri zinazopakana.
Katika hatua nyingine MhandisiKalobelo amewapongeza Viongozi wa Wilaya ya Kilombero pamoja na Halmashauri ya Mlimba Wilayani humo kwa kutoa Mkopo wa zaidi ya shilingi milioni 820kwa vikundi 99 vya wanawake, Vijana na watu wenye ulemavu ikiwa ni mkopo usio na ribawafedha zinazotokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri hiyo kuanzia Mwezi Julai hadi Oktoba mwaka huu.
Amesema huo ni mfano wa kuigwa kwa halamashauri nyingine za Mkoa huo huku akiwataka waliopata Mkopo huo usio na riba kuhakikisha wanarejesha fedha hizo kwa wakati ili wengine waweze kukopeshwa lakini pia wametakiwa kupitia fedha hizo kuanzisha miradi yenye tija.
Ili kuhakikisha vikundi hivyo vinapata tija, Mhandisi Kalobelo amewataka Wataalamu katika Halmashaurizote kuvisaidia vikundi katika kuandika Maandiko ya miradi yenye tija kwa vikundi vyenyewe, kwa jamii na taifa kwa ujumla huku akibainisha kuwa hilo ndilo lengo la Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Dkt. John Pombe Magufuli.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Ulanga Ngollo Malenya mmoja wa Wakuu wa Wilaya walioshiriki maadhimisho hayo, aliwataka wanawake kuendelea kuwa waaminifu kwenye mikopo ya fedha za Serikali kwa kuwa wameonekana ni waaminifu zaidi katika marejesho ya fedha hizo ukilinganisha na wanaume.
Aidha, kuhusu uzinduzi wa kilimo Ngollo Malenya amesema amejifunza mengi katika sherehe hizo ikiwa ni pamoja na mbinu mpya za kilimo cha umwagiliaji cha zao la mpungahususan kupanda zao la mpunga kkwa kutumia mafungu.
Naye, Katibu Tawala Msaidizi Mkoani humo, anayeshughulikia masuala ya kilimo Dkt. Rozalia Rwegasira pamoja na kuwakumbusha wakulima kuwa msimu w kilimo umeanza huku akiwataka wakulima kutambua kuwa kilimo ni Biashara kama zilivyo biashara nyingine hivyo ni wajibu wao kukithamini na kukienzi, kulima kwa malengo na kufuata kanuni bora za kilimo.
Aidha, aliwakumbusha Maafisa Kilimo kuanza kuandaa ratiba ya kuwatembelea wakulima na kutoa ushauri unaohitajika ili wakulima waweze kuzalisha kwa tija na kwamba maafisa kilimo hawahitajika kukaa Ofisini hususan katika kipindi hiki cha kilimo.
Baadhi ya Wakurugenzi walioshiriki maadhimisho hayo akiwemo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Gairo Agnes Mkandya amesema maadhimisho hayo yamemwongezea ujuzi huku akiahidi akipendezwa na kilomo cha zao la kokoa linalolimwa katika halmashauri hiyo na kwamba ameazimia pia zao hilo kulimwa katika halmashauri ya Gairo.
Maadhimisho hayo ya uzinduzi wa Msimu wa Kilimo Mkoani Morogoro ambayo kwa mwaka huu yalikuwa na kaulimbiu “Kilimo endelevu kwa lishe Bora, Ajira na Maendeleo ya Viwanda”Mwakani yanategemewa kufanyika katika Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro Wilayani Morogoro.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.