Mkoa wa Morogoro kutenga Ekari 30,000 kwa ajili ya wafugaji.
Mkoa wa Morogoro umetenga eneo la Hekari elfu 30 kwa ajili ya wafugaji ikiwa ni moja ya njia ya kutatua na kupunguza kama sio kukomesha kabisa changamoto ya migogoro baina ya wakulima na wafugaji Mkoani humo ambapo pia wafugaji watatakiwa kupanda nyasi za malisho eneo hilo ili kuokoa mifugo yao nyakati za ukame.
Kauli hiyo imetolewa Julai 16, 2022 na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela wakati wa Mkutano wa wadau wa mifugo Mkoani humo uliofanyika katika ukumbi wa Chuo Kikuu cha Waislam cha Morogoro (MUM) katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela akizungumza wakati wa Mkutano na wadau wa Mifugo Mkoani humo Julai 16 mwaka huu katika ukumbi wa Chuo Kikuu cha waislam cha Morogoro.
Martine Shigela amesema kuwa katika kuonesha jitihada za kukabiliana na migogoro ya wakulima, wafugaji na watu wa uhifadhi wa misitu hapa nchini Serikali ya Mkoa huo itatenga eneo hilo ili wafugaji waweze kuendesha shughuli zao kwa uhuru zaidi.
“Mhe. Waziri tuna eneo lenye ukubwa wa ekari elfu 30 na tutalitenga kwa ajili ya wafugaji na kuwekewa mpango maalum wa kulipima ili wafugaji wetu waweze kuendesha shughuli zao kwa kulimiliki eneo hilo kihalali” amesema Shigela.
Wenyeviti na Wakurugenzi wa Hamashauri za Mkoa wa Morogoro wakifuatilia Maelekezo mbalimbali ya viongozi wakuu wa Serikali wakati wa Mkutano wa wadau wa Mifugo Mkoani Morogoro.
Katika hatua nyingine Martine Shigela amemuomba Waziri wa Mifugo na Uvuvi Dkt. Mashimba Ndaki kuitisha kamati ya wanasheria ili kuweza kukaa pamoja na kupata fursa ya kutafisiri upya sheria ya faini ya mifugo pale inapobainika kuwa wafugaji wamevunja sheria kwani kwa sheria zilizopo sasa zinaukakasi katika kuzitekeleza, zipo zinazotaja faini ya shilingi Tsh. 100,000/= kwa tukio na ile inayotaka kuhesabu idadi ya mifugo na kila mfugo kulipiwa shilingi 100,000/=.
Baadhi ya wadau wa Mifugo wakiwa katika Mkutano huo.
Kuhusu mipaka tofauti tofauti iliyowekwa kati ya 2012, 2015 na 2017 katika Bonde oevu la Kilombero kutenganisha baina ya uhifadhi wa Bonde hilo na shughuli za kibinadamu amesema uamuzi wa sasa ni kufuata mpaka ule uliotolewa na Kamati ya Mawaziri nane (8) mpaka wa 2017 lengo hapo ni kuondoa migongano ya sasa kutojua kuwa mifugo iko nje ya hifadhi ama la au kutojua kuwa shughuli za mkulima fulani zinafanyika ndani ya uhifadhi wa Bonde ama la, huku akifungua milango kuwa kama kuna mapendekezo mengine, yatolewe lakini wakati mpaka huo unaendelea kuheshimiwa.
Kwa upande wake Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Mashimba Ndaki pamoja na kupongeza jitihada hizo za Mkoa huo amewataka Wakuu wa Mikoa hapa nchini kufanya mikutano na majukwaa kundi hilo la wafugaji na wadau wengine wa ugaji ili kutatua kwa pamoja kero zinazowakabili.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Mashimba Ndaki akitoa onyo la kutokuingiza Mifugo kwenye maeneo ya uhifadhi kwa wafugaji katika Mkutano na wadau wa Mifugo.
Aidha, Waziri huyo wa Mifugo na Uvuvi amesisitiza kuwa ni muhimu pande zote kuheshimu misingi ya kisheria iliyowekwa ili kuleta uwajibikaji baina ya pande zote hatimaye kuondoa malalamiko ya wafugaji yaliyopo likiwemo la baadhi ya watumishi wa Serikali wasio waaminifu, ingawa amesema, malalamiko hayo kwa kiasi kikubwa yamepungua ukilinganisha na hapo awali.
“Sasa tusaidiane kuwabaini hao wasio waaminifu na waliokuwa kero kwetu sisi wafugaji ili tuchukue hatua stahiki lakini na Ninyi wafugaji muache mara moja tabia ya kupeleka mifugo hifadhini” amesisitiza Dkt. Ndaki.
Mbunge wa Jimbo la Morogoro Kusini Mhe. Innocent Karogeresi akizungumza wakati wa Mkutano huo.
Mbunge wa Jimbo la Mikumi Mhe. Dennis Londo kwa niaba ya Wabunge wengine wa Mkoa wa Morogoro ameiomba Serikali kuona kama kuna uwezekano na hakuna athari kubwa iruhusu mifugo kuingia kwenye maeneo ya mapori ya akiba (TFS) kwa hoja kuwa mifugo haili miti bali inakula majani, hivyo ili kupunguza changamoto ya wafugaji kukosa maeneo ya marisho, Serikali ikae na Taasisi zake kutazama upya pendekezo hilo.
Mbunge wa Jimbo la Mikumi Mhe. Denis Londo ambaye pia ni Katibu wa Wabunge wa Mkoa wa Morogoro akiwasilisha salamu za Wabunge wa Mkoa huo katika Mkutano huo.
Naye Kalaika Motosyo ambaye ni mwenyekiti wa chama cha wafugaji kata ya Parakuyo kwa niaba ya wadau wengine wa mifugo amesema suala la kuvisha hereni mifugo kwa minajiri ya kutambulika na kupunguza migogoro ni jambo jema hivyo, ameiomba Serikali kuendelea kutoa elimu ili kuleta ufanisi wa zoezi hilo la uwekaji heleni mifugo.
Wadau wa Mifugo wa Mkoa wa Morogoro wakifuatilia kwa karibu maelekezo ya Serikali ya kuwapatia wafugaji Ekari elfu 30 kwa ajili ya shughuli za malisho ya Mifugo Mkoani humo kama sehemu ya kutatua migogoro.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.