Mkoa wa Morogoro umejipanga kukuza uchumi wa Mkoa na nchi kwa ujumla kwa kujikita kwenye sekta ya kilimo chenye tija, ufugaji wa kisasa pamoja na kuhifadhi mazingira.
Hayo yamebainishwa Novemba 13 mwaka na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima wakati akifungua kikao cha wadau wa kilimo, mifugo na mazingira Mkoa wa Morogoro kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa hoteli ya Morena iliyopo Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima akizungumza na wadau wa kilimo wakati wa kikao cha wadau wa kilimo, mifugo, uvuvi na mazingira Mkoa wa Morogoro.
Mkuu huyo wa Mkoa amesema Mkoa wa Morogoro unaendelea na jitihada za kuhifadhi na kulinda mazingira kwa kuwa ni kichocheo cha maendeleo ya kiuchumi na kijamii hapa nchini. Aidha, amesema utunzaji wa mazingira hususan vyanzo vya maji ndani ya Mkoa huo utawahakikishia upatikanaji wa umeme kwenye Bwawa la Mwalimu Nyerere ambalo linatarajia kuzalisha Megawati zaidi ya 2,000.
“...wao wajue jinsi ambavyo sisi Morogoro tunavyopigana kuhifadhi na kutunza mazingira kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya Taifa hili... lazima sisi watu wa Morogoro tulinde vyanzo vya maji na kuhifadhi mazingira...” amesema Mkuu wa Mkoa.
Kwa upande wa sekta ya kilimo, Mkuu wa Mkoa amesema Mkoa huo umepanga kuzalisha mazao ya biashara likiwemo zao la parachichi, ambapo wakulima 20 na Maafisa ugani wataenda Mkoa wa Njombe kupata mafunzo ya zao hilo na watapatiwa miche ya parachichi 50,000 kwa ajili ya kupandwa katika Tarafa ya Nongwe Wilayani Gairo.
Sambamba na hayo, Mhe. Adam Malima amewahimiza wakulima wa Mkoa huo kujiunga kwenye vyama vya ushirika ili waweze kupatiwa mikopo na pembejeo za kilimo zikiwemo mbolea, mbegu na zana za kulimia kutoka Taasisi za mikopo za Mkoa huo.
Kwa upande wake Meneja wa taasisi ya Southern Agricultural Growth Corridor of Tanzania – SAGCOT Mkoa wa Morogoro Bw. James Banga amesema kikao hicho cha wadau wa Kilimo, Mifugo, Uvuvi na Mazingira kimelenga kufanya mapitio ya maazimio ya kikao kilichofanyika 2022 ili kuboresha utunzaji wa Mazingira, kilimo chenye tija kinacholinda mazingira pamoja na uvuvi bora.
Aidha, ameongeza kuwa hali ya utunzaji wa Mazingira katika Mkoa huo imeimarika kutokana na nguvu kubwa ya usimamizi wa viongozi wa Mkoa huo pamoja na utayari wa Wananchi katika kulinda mazingira kwa kuhamasika kulima mazao ya viungo mbalimbali ambayo hayaharibu mazingira.
Nao baadhi ya wakulima akiwemo Mwenyekiti wa vyama vya ushirika – AMCOS za miwa Bonde la Kilombero Bw. Bakari Mkangamo amewaasa wakulima kujiunga na vyama vya ushirika ili kupata urahisi wa pembejeo za kilimo pamoja na mikopo.
Wajumbe wa kikao hicho wameazimia mambo mbalimbali ikiwemo Mkoa kujikita kwenye kilimo cha mazao ya viungo likiwemo zao la karafuu huku Mkoa ukisaini hati ya makubaliano ya kiutendaji na Asasi za kiraia na Sekta binafsi kwa ajili ya kufanya mapinduzi ya kilimo hususan kilimo mazao, mifugo, uvuvi na mazingira.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.