MKOA WA MOROGORO WAJIPANGA KUTANGAZA VIVUTIO/ KUKUZA UTALII.
Serikali Mkoani Morogoro kwa sasa inajipanga kwa ajili ya kuweka mazingira na mikakati madhubuti ya kutangaza vivutio vilivyopo mkoani humo kwa lengo la kukuza Sekta ya Utalii na kuingizia mkoa huo na taifa kwa ujumla mapato yatokanayo na sekta hiyo.
Hayo yamebainishwa Julai 26, 2024 na Afisa Maliasili wa Mkoa huo Bw. Joseph Chuwa wakati wa kikao cha wadau mbalimbali wa utalii kilichofanyika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro ili kujadili na kuandaaa kongamano la wadau wa utalii wa Mkoa huo.
Bw. Chuwa amesema, katika kikao hicho wameweka mikakati ya kuhamashisha utalii kupitia makala ya Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yaani Royal Tour ambayo imeleta uhai mkubwavkatika sekta ya utalii hiyo itasaidia Mkoa wa Morogoro uliobarikiwa vivutio vingi vya utalii kufadika kimapato kwa faida ya wanamorogoro na watanzania wote kwa jumla.
".. Lengo letu hapa ni kuweka mkakati wa kuona namna gani tunatumia fursa hizi pia mkakati wa kuona namna gani tutaweza kutumia vivutio tulivyonavyo ili kufungua utalii ndani ya Mkoa ..." Amesema Bw. Joseph Chuwa.
Aidha Bw. Chuwa ametoa wito kwa Sekta binafsi Mkoani humo kuchangamkia fursa ya ujio wa treni ya kisasa (SGR) ambayo itatumika sana kuleta watalii wengi ndani ya Mkoa huu hivyo wananchi wawekeze katika mahoteli makubwa ya kitalii yatakayoweza kutoa huduma nzuri kwa wageni.
Kwa upande wake Balozi wa Utalii Tanzania ambae pia ni Mkurugenzi wa NABEC Company limited Bi. Nangasu Warema katika kikao hicho amesema kuna umuhimu wa Wanamorogoro kutambua faida ya utalii hivyo kama Sekta ya utalii ina jukumu la kutoa elimu kwa wananchi hao juu ya faida ya utalii na kuweza kujihusisha katika Sekta hiyo ili kujiingizia kipato na kukidhi maisha yao.
Naye, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi kanda ya Mashariki ( TANAPA) Bw. Fedrick Malisa katika hatua ya kukuza utalii Mkoani humo ametoa ushauri wa kuweka video fupi katika treni ya kisasa (SGR) pia katika mabasi kwa lengo la kuvitangaza vivutio vilivyopo Mkoani humo ili kuweza kuwavutia watalii kwa wingi.
Sambamba na hayo mdau kutoka kampuni ya SEE AFRICA SATARIS Bi. Eda Kapinga amesema Serikali ya Mkoa ina umuhimu wa kujikita katika Sekta ya utalii ambapo itawashawishi na kuleta chachu kwa wananchi wa Mkoa huo kujihusisha katika masuala ya utalii.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.