Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Ifakara Bi. Lena Nkaya kushirikiana na Madiwani wa Halmashauri yake katika kusimamia miradi ya maendeleo inayotekelezwa ndani ya Halmashauri hiyo kwa lengo la kuongeza chachu ya ubora na ukamilishaji wa miradi hiyo kwa wakati.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Malima (katikati) akiwa pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Kilombero Mhe. Danstan Kyobya (kulia), Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Ifakara Bi. Lena Nkaya na viongozi wengine kwenye eneo la ujenzi wa jengo jipya la Halmashauri ya Mlimba.
Mhe. Malima ametoa agizo hilo Juni 9 mwaka huu wakati akizungumza na Madiwani kwenye Mkutano maalum wa kupitia hoja za Mkaguzi Mkuu wa Serikali - CAG uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri hiyo.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Malima akitoa maelekezo wakati akikagua ujenzi wa jengo jipya la Halmashauri ya Mlimba.
Akiongea wakati wa Mkutano huo Mkuu wa Mkoa amesema suala la usimamizi wa miradi katika Halmshauri hiyo ni wa kusua sua na kubainisha kuwa Diwani ndiye msimamizi wa miradi ya maendeleo katika eneo husika.
Kwa sababu hiyo, Mkuu wa Mkoa amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Ifakara kuratibu namna Madiwani watakavyosimamia miradi katika maeneo yao.
"...sasa msimamizi mkuu wa miradi ni Mhe. Diwani, kwa hiyo Mkurugenzi nisikilize vizuri sana hili ni agizo la Mkuu wa Mkoa mimi, kwamba muorodheshe miradi yote inayo kwama kisha kwenye kila mradi kuwe na wasimamizi Madiwani wanne wanne..."
amesema Mkuu wa Mkoa.
Muonekano wa jengo jipya Wilayani Kilombero ambalo linaendelea kujengwa.
Aidha, Mhe. Adam Malima ametaja miradi ambayo Madiwani hao wanatakiwa kuisimamia kuwa ni pamoja na miradi ya maji, afya, elimu na barabara za TARURA.
Akisisitiza zaidi, Mhe. Malima amesema Mkurugenzi wa Halmashauri atahusika katika kuratibu na kugharimia safari za Madiwani hao ili mradi tu wahe. Madiwani waweze kufanikisha zoezi hilo.
Kwa upande wake Mkaguzi wa nje na mdhibiti wa Hesabu za Serikali Mkoa wa Morogoro CPA Peter Mwabwanga amemshukuru na kumpongeza Mkuu wa Mkoa katika harakati zake za kuzirekebisha Halmshauri za Mkoa huo katika ukusanyaji wa mapato na ukamilishaji wa miradi ya maendeleo na kukili kuwa juhudi hizo zinaonesha nia yake njema ya kuwaletea Wananchi wa Mkoa huo maendeleo.
Nae Katibu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Morogoro Ndg. Solomon Kasaba amewataka Madiwani wa Halmashauri hiyo kushirikiana na Uongozi wa Mkoa na Wilaya katika harakati za kuwaletea Wananchi maendeleo bila woga.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.