Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela ameutaka Uongozi wa Kiwanda cha Sukari cha Kilombero kushughulikia malalamiko ya wakulima wanaopeleka miwa yao katika kiwanda hicho ikiwemo madai ya ucheleweshwaji wa kuvuna zao hilo jambo ambalo linatajwa kurudisha nyuma jitihada za wakulima hao.
Shigela ameyasema hayo April 23, mwaka huu wakati wa mkutano na Uongozi wa Kiwanda cha Sukari cha Kilombero, Viongozi wa vyama vya ushirika vya wakulima wa miwa, wakulima wa zao la miwa Pamoja na viongozi wa Halmashauri za Wilaya ya Kilosa na Kilombero uliofanyika katika Ukumbi wa mikutano wa Chuo cha Sukari Cha Kilombero.
Shigela ameutaka Uongozi wa Kiwanda hicho kuhakikisha miwa inayolimwa na wakulima hao inachukuliwa na kiwanda hicho na pasiwepo na miwa inayotupwa.
“nielekeze Uongozi wa Kiwanda ufanye kinachowezekana kuchukua miwa ya wakulima. Sitarajii mwaka huu kuona tena miwa inatupwa, Kama kiwanda kina uwezo wa kuchukua kiasi cha miwa kilicholimwa basi uwekwe utaratibu kiasi hicho chote kichukuliwe ”. Amesema Shigela.
Akifungua Mkutano huo, Mkuu huyo wa Mkoa amewataka wakulima wa miwa katika bonde la Kilombero kumweleza bila kificho changamoto zinazowakabili katika kilimo hicho ili kuondosha malalamiko kati yao na Kiwanda cha Sukari Kilombero jambo ambalo linaweza kuzorotesha uzalishaji wa zao hilo.
Wakiongea mbele ya Mkuu huyo wa Mkoa baadhi ya wakulima wa zao hilo wamesema miongoni mwa changamoto wanazokutana nazo ni Pamoja na tozo katika vikundi vya ushirika vya wakulima wa miwa, ubaguzi wakati wa kuvuniwa mazao yao kutoka shambani na kuchukuliwa kiasi fulani cha miwa kuingizwa kiwandani na kingine kutupwa.
Changamoto nyingine walizozitaja ni kukosekana kwa uwazi wa thamani ya miwa ambayo ndio hutengeneza malipo ya mkulima sambamba na kupewa kazi ya kupeleka miwa kiwandani kwa watu wasio na sifa stahiki.
Kufuatia changamoto hizo zilizotolewa na wakulima hao, Mkuu wa Mkoa Martine Shigela amewataka viongozi wanaohusika akiwemo Mrajisi msaidizi wa vyama vya ushirika Mkoa wa Morogoro Keneth Shemdoe Pamoja na Meneja wa huduma kwa wakulima kutoka kiwanda cha Sukari Kilombero Job Zahoro kutafuta suluhisho la haraka la malalamiko hayo.
Awali akitoa ufafanuzi katika baadhi ya changamoto zilizotajwa na wakulima hao, Meneja huduma kwa wakulima Kiwanda cha Sukari Kilombero Job Zahoro amesema kiwanda kitanzingatia vigezo stahiki katika kuwapata wakandarasi watakaojihusisha na shughuli za ubebaji wa miwa kupeleka kiwandani ili kuondoa changamoto zilizojitokeza.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kilombero Hanji Godigodi amewaomba viongozi wa vyama vya ushirika Pamoja na Mrajisi wa Kanda kufuata kanuni na sheria sambamba na kumuogopa Mungu wakati wa utekelezaji wa majukumu yao ili kulinda maslahi ya wakulima akibainisha kwamba kazi ya Kilimo ni ngumu.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Alhaji Majid Mwanga ameahidi kuwashughulikia viongozi watakaozembea kutatua changamoto zinazowakabili wakulima kupitia vyama vya ushirika vya wakulima wa miwa.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.