Mtu mmoja amefariki dunia na wengine 85 kujeruhiwa baada ya roli ya kampuni ya Yapi markez inayojenga reli ya kisasa SGR kuigonga treni ya abiria ya reli ya kati iliyokuwa safarini kutoka Kigoma kuelekea Jijini Dar es salaam.
Hayo yamebainishwa Julai 22, Mwaka huu na Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro Fortunatus Muslimu alipofika eneo la ajali lililopo kidete Wilaya ya Kilosa Mkoani Morogoro ambapo amesema ajali hiyo ilitokea katika makutano ya reli na barabara inayotumika kupitisha vifaa vya ujenzi wa reli ya kisasa.
Muslimu amemtaja aliyefariki katika ajali hiyo kuwa ni Dereva wa roli ambaye pia ni mfanyakazi wa Shirika la Reli Tanzania aliyefahamika kwa jina la Jerald Marandu aliyeigonga treni hiyo na kupelekea mabehewa mawili ya treni kuhama njia yake.
‘’…Treni hii ilikuwa inatoka kigoma kwenda Dar es salaam baada ya kufika katika eneo hili ajali ilitokea ambapo roli iliigongo treni, kutokana na kuanguka jumla ya abiria 85 wamejeruhiwa na mmoja amefariki ambaye ni dereva wa roli…’’ amesema Muslimu.
Aidha, Muslim ametoa wito kwa madereva kuchukua tahadhali katika maeneo ambayo ujenzi wa reli ya kisasa unaendelea ili kuepusha ajali zinazoweza kuepukika na kuleta madhara katika ujenzi ikiwa ni pamoja na kusimama kwa ujenzi wa barabara na kazi nyingine.
Awali akiwasilisha salamu za pole kutoka kwa Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martine Shigela amewasilisha pole za Rais kwa familia ya wafiwa, abiria wote waliokuwa wakisafiri, Kampuni ya Yepi markez, Shirika la Reli Tanzania -TRC na watanzania wote kwa jumla.
Sambamba na hayo, Shigela ametoa shukrani kwa Kampuni ya Yepimarkez kwa jitihada walizozifanya za kusaidia kuleta mabasi kwa ajili ya kubeba majeruhi na kuwafikisha katika Hospitali ya Wilaya ya Kilosa kwa ajili ya kupatiwa huduma ya kwanza, lakini pia kulinda mali za abiria kutopotea.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro baada ya kutembelea eneo la ajali alifika Hospitali ya Wilaya ya Kilosa ambapo majeruhi wa ajali hiyo walikuwa wamepelekwa kupata matibabu ya awali na kuwajulia hali huku akiagiza jeshi la polisi kulinda mizigo yote ya wahanga wa ajali hiyo na kisha kuwafikishia ikiwa salama.
Naye Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala wa TRC Amina Lumuli amesema kazi zinazoendelea sasa ni kuyafanyia uchunguzi mabehewa 12 kati ya 14 ya treni hiyo kama yako salama kuweza kuendelea na safari, kurekebisha njia ndogo ambayo imepata hitirafu na kunyanyua mabehewa mawili yaliyoanguka pamoja na kichwa cha treni.
Treni hiyo iliyokuwa inatoka Kigoma kwenda Dar es Salam ilikuwa na mabehewa 14 na zaidi ya abiria 1000, kati ya majeruhi hao 85, majeruhi 70 ni watu wazima na 15 ni watoto.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.