Morogoro, China kushirikiana kukuza kilimo.
Mkoa wa Morogoro na nchi ya China zimekubaliana kushirikiana ili kukuza Sekta ya Kilimo Mkoani humo kwa lengo la kuinua uchumi wa wakulima, Mkoa na Taifa kwa ujumla.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima akipokea zawadi kutoka kwa Mhadhiri wa Chuo cha Kilimo - CAU cha nchini China Prof. Li Xiaoyun.
Hayo yamebainishwa Novemba 27,2023 na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima alipokutana na Viongozi wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha CAU cha nchini China walipomtembelea Mkuu wa Mkoa huo Ofisini kwake kwa ajili kuangalia maendeleo ya shamba darasa katika kijiji cha Mtego wa Simba kilichopo Wilaya ya Morogoro.
Katika mazungumzo yao Mkuu wa Mkoa amesema Mkoa umepanga kulima mazao matano ya Kimkakati ya biashara ambayo ni Karafuu, Kahawa, Kokoa, Parachichi na Michikichi lengo ikiwa ni kuinua Uchumi wa wakulima wadogo.
"...nataka wakulima walime mazao yatakayoisaidia familia, kwa hiyo nimeazisha kilimo cha mazao matano, zao la karafuu, Kakao, Michikichi, Parachichi na Kahawa..." amesema Mkuu wa Mkoa.
Aidha, Mhe. Adam Malima amewaomba viongozi hao kushirikiana kufanya utafiti kwenye sekta hiyo ya kilimo ili kuongeza tija ya uzalishaji wa mazao hayo.
Kwa upande wake Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha CAU cha nchini China Prof. Li Xiaoyun amemshukuru Mkuu huyo wa Mkoa kwa kutoa ushirikiano wa kutosha kwao na kukubali kushirikiana katika sekta hiyo ya kilimo.
Aidha, amempongeza Mhe. Adam Malima kwa maono mazuri aliyonayo juu ya kilimo na kumhakikishia kuwa Chuo CAU kipo tayari kumpokea kwa ajili ya kuongeza uzoefu zaidi katika Sekta hiyo ya Kilimo.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.