Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Ali Malima amesema kuwa Morogoro imejipanga kuendelea kuwa kinara katika shughuli za kilimo hususan zao la mpunga ambapo huchangia kwa kiasi kikubwa katika biashara, viwanda na shughuli za kijamii ili kukuza uchumi wa Mkoa na Taifa.
Mhe. Malima ametoa kauli hiyo Novemba 2, 2023 katika mkutano wa msemaji mkuu wa serikali na waandishi wa Habari uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro.ukiwa na lengo la kutangaza mafanikio ya serikali ya awamu ya sita ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Mkoani humo.
Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa amesema kuwa dhamira ya kilimo Mkoani humo ni kuongeza tija ya uzalishaji kutoka tani laki 9 hadi tani Mil. 1.5 za mpunga ili kujiweka katika mazingira mazuri ya usalama wa chakula kwa watu mil 3.2 kwa mujibu wa sensa ya watu na Makazi ya mwaka 2022 waliopo Mkoani humo, hivyo wananchi wanatakiwa kujikita katika shughuli mbalimbali za maendeleo ikiwemo biashara, viwanda na shughuli za kijamii.
“…Mkoa wa Morogoro ndiyo namba moja katika uzalishaji wa mpunga ambapo sasa hivi tumefikia uzalishaji wa tani laki 9 na malengo yetu kufikia tani milioni 1.5 kwa mwaka…”amesema Mhe. Adam Malima
Sambamba na hilo, Mhe. Adam amebainisha kuwa wananchi wanapaswa kujua miradi muhimu inayotekelezwa katika maeneo yao na serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuzingatia uwekezaji wa sekta za umma na sekta binafsi ili kukidhi mahitaji ya wananchi wa Mkoa huo.
Katika hatua nyingine, Mhe. Malima amemshukuru Mhe. Rais kwa kuuheshimisha Mkoa wa Morogoro kuwa Mkoa wa Kimkakati ambapo miradi ya kimkakati ikiwemo Barabara kuu na reli ya kisasa ya umeme zinazounga Mkoa wa Kibiashara (Dar es Salaam) na Mkoa wa Makao Makuu ya serikali (Dodoma) hivyo, kutasaidia kukuza uzalishaji wa kilimo, Viwanda na shughuli za kibiashara sambamba na kuongeza pato la Taifa.
Kwa upande wake, Msemaji Mkuu wa Serikali, Bw. Mobhare Matinyi amesema kuwa Mhe. Rais amewafikia wananchi katika hatua mbalimbali ikiwemo kutoa fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo hususan Barabara ambayo ndiyo chachu ya maendeleo katika sekta zilizopo Mikoani na Nchi kwa ujumla, na kuwataka wakurugenzi kufuata maelekezo ya serikali ili kuendana na kasi ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro Bi. Joanfaith Kataraia amesema serikali ya awamu ya sita kwa kipindi cha miaka miwili imetoa zaidi ya Tsh. Bil. 64 katika kutekeleza miradi ya maendeleo ya Halmashauri hiyo ikiwemo sekta ya afya, elimu na utawala ambapo hapo awali wananchi walilazimika kutembea umbali wa kilometa 200 kufuata huduma hizo, hivyo serikali imetatua mahitaji muhimu ya wananchi wa Halmashauri hiyo.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.