Uongzi wa Serikali ya Mkoa wa Morogoro umesema utaendelea kukomesha migogoro ya Ardhi, pamoja na mapigano baina ya wakulima na wafugaji ndani ya Mkoa huo kwa lengo la kumuenzi alieyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli aliyefariki dunia Machi 17 mwaka huu.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Loata Ole Sanare wakati wa Kongamano maalum la kuomboleza kifo cha hayati Dkt. John Pombe Magufuli lililofanyika Machi 23 mwaka huu katika viwanja vya Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Mvomero na kuhusisha wananchi na viongozi mbalimbali wa dini na Serikali.
Loata Sanare amesema moja ya kazi kubwa aliyokuwa amepewa na hayati Dkt. John Pombe Magufuli wakati wa uteuzi wake ni kumaliza migogoro kati ya wakulima na wafugaji iliyokuwa ikiendelea Mkoani humo hususan katika Wilaya za Mvomero na Kilosa.
“Nashukuru mungu tulipokutana ametoa pongezi za kutosha kwangu na kwa viongozi wote wa Mkoa wa Morogoro kwamba angalau kwa mwaka mmoja tu tumeweza kudhibiti na kuhakikisha hawawezi kupata taarifa kubwa ya migogoro, kazi hii sikufanya mimi, Mkuu wa Wilaya, wamefanya viongozi wetu wenyeviti na watendaji wa vijiji” alisema Sanare.
Loata Sanere amesisitiza kuwa ili kumuenzi hayati Dkt. John Pombe Magufuli, Mkoa wa Morogoro hauna budi kusimamia kwa nguvu zote Ulinzi wa watu na mali zao katika Mkoa huo pamoja na amani iliyopo kwa Serikali kushirikiana na wananchi pamoja na wadau mbalimbali ndani ya Mkoa huo.
Akihitimisha hotuba yake, Loata Sanare amesema pamoja na kuendelea kudhibiti migogoro ya wakulima na wafugaji, Dkt. John Pombe Magufuli ataenziwa kwa kuendeleza ujenzi wa shule ya Sekondari ya Kumbukumbu ya Sokoine inayojengwa Wilayani Mvomero ambapo tayari kabla ya umauti kumkuta alishatoa shilingi 4 Bil. Kati ya shilingi Bil. 12 zinazohitajika kukamilisha ujezi huo, kisha utajengwa mnara au sanamu ya hayati Waziri Mkuu Moringe Sokoine aliyefariki eneo hilo kwa ajali ya gari.
Wakitoa salamu za maombolezo wawakilishi wa wananchi Wilayani Mvomero akiwemo Mwenyekiti wa waendesha Pikipiki – Bodaboda Ndg. Rashid Mohamed, amesema hayati Dkt. John Pombe aliwasaidia bodaboda hao kutambua sheria za barabarani na kuwapatia fedha za mkopo kwa riba nafuu ambayo iliwasaidia kujikimu kimaisha na familia zao.
Naye, Katibu wa wafugaji katika Mkoa wa Morogoro Joshua Lugaso amesema kuwa hayati Dkt. John Pombe Magufuli amewasaidia sana wafugaji kwa kuwapatia masoko ambapo viwanda vya nyama zaidi ya vitatu vimejengwa kikiwemo kiwanda cha Longido ambacho kina uwezo wa kuchinja mbuzi 1000 na Ng’ombe 500 kwa siku.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Albinus Mgonya amebainisha baadhi ya mambo ambayo watamkumbuka shujaa huyo kwa kuchapakazi, kuwa wazalendo kwa nchi yao, kupinga rushwa, kupenda maendeleo na kupenda haki pamoja na mabadiliko chaya kwa manufaa ya jamii.
Sambamba na hayo, Mgonya ametoa wito kwa wananchi wa Mvomero kuenzi mambo yote mazuri aliyoyafanya hayati Dkt. John Pombe Magufuli, ikiwa ni pamoja na kuepuka viashiria vyovyote vya uvunjifu wa amani katika jamii, kufanya kazi kwa bidii, kutoa huduma bila upendeleo na kutii maagizo ya Serikali.
MWIISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.