Mkoa wa Morogoro umetajwa kuwa kitovu cha Utalii wa ndani hapa nchini kwa siku za karibuni kutokana na urahisi wa kufikika kutoka maeneo mbalimbali ya Tanzania baada ya Serikali ya awamu ya sita chini ya Mhe. Dkt, Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kufanya uwekezaji mkubwa katika sekta ya miundombinu.
Hayo yamebainishwa Aprili 3, 2025 na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima Ofisini kwake wakati anaongea na Wajumbe wa Chama cha Maafisa Mawasiliano wa Serikali (TAGCO) waliofika kujitambulisha Ofisini kwake na kumweleza kuwa watakuwa na kikao kazi ndani ya Mkoa huo.
Amesema, uwekezaji Mkubwa uliofanywa na Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye sekta ya miundombinu hususan ujenzi wa Reli ya mwendo kasi - SGR umeleta chachu na kufanya Mkoa huo kufikika kiurahisi na hivyo kurahisisha pia sekta ya Utalii na kuwafanya watalii kushawishika kuja mkoani humo kwa ajili ya kutalii.
"Mkoa wa Morogoro sasa hivi ndio mwelekeo mkubwa wa utalii wa ndani Tanzania kwa sababu unafikika kiurahisi kwa uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali wa Treni ya mwendo kasi - SGR" Amebainisha Mhe. Adam Malima.
Pamoja na kuwapokea na kuwakaribisha Mkoani humo, Mkuu huyo wa Mkoa amewataka Maafisa hao kutumia fursa hiyo baada ya kikao chao kutembelea vituo vya utalii vilivyoko mkoani humo ikiwemo Mbuga ya wanyama ya Mikumi na milima ya Udzungwa ambayo ina vivutio lukuki kama vile maporomoko ya maji, misitu na viumbe hai mbalimbali vya kuvutia.
Sambamba na hayo amewatakia Maafisa Mawasiliano hao mkutano mwema huku akiwataka kujadiliana na kupeana uzoefu ili kuboresha taaluma yao katika kutoa taarifa za Serikali kwa wananchi wake kwa manufaa ya Taifa la Tanzania.
Chama hicho cha TAGCO kitakuwa na Mkutano wake wa kawaida Mkoani humo kwa muda wa siku saba (7) katika hoteli ya Morena iliyopo Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro mkutano unaotarajiwa kufanyika Aprili 8 - 12, 2025 na ambao utakuwa na washiriki wasiopungua mia tano (500).
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.