Morogoro kuwa kitovu cha uzalishaji wa mazao ya viungo.
Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro Dkt. Mussa Ali Mussa amesema mkoa wa Morogoro umejipanga kwa ajili ya kilimo cha mazao ya viungo hususan Karafuu ili kuongeza kipato cha Wananchi wa Mkoa huo na taifa kwa jumla lakini pia lengo likiwa ni kurudisha uoto wa asili katika milima ya Urugulu.
Dkt. Mussa Ali Mussa ametoa kauli hiyo Januari 25, 2024 wakati wa kikao cha Wizara ya Kilimo cha kutambulisha mradi wa uzalishaji wa miche ya mikarafuu kilichofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo kikao kilichoratibiwa kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo.
Amesema, kwa kushirikiana na mashirika mengine yakiwemo Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) na Mamlaka ya usimamizi wa Wanyama Pori Tanzania (TAWA) watatoa bure kwa wananchi miche ya mazao ya Viungo ikiwemo miche ya mikarafuu ili waweze kupanda katika milima ya Uluguru zao litakalokuwa rafiki kwao hivyo kusaidia kutunza mazingira ya milima hiyo.
"milima ya Uluguru inakabiliwa na uharibifu wa mazingira kwa kukata miti ovyo, kwa kupanda mazao hayo ya Karafuu itapelekea wananchi kutokata miti hiyo kwa kuwa inawaingizia kipato na wakati huo itahifadhi mazingira". Amesema Dkt. Mussa.
Katika Hatua nyingine Dkt. Mussa amesema kuwa, Mkoa huo umeanza kujenga maghala ya kuhifadhia karafuu ili kuwa na sehemu moja ya kuuzia zao hilo, na kusaidia Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro kuweza kusimamia na kukusanya mapato yake vizuri.
Aidha, amesema, Wananchi wameweza kuhamasika na kuanza kupanda miche ya mikarafuu pamoja na kuzalisha miche hiyo si chini ya laki 4, hivyo kama mkoa wanajipanga ili kwenda kununua miche hiyo iliyozalishwa na wananchi na kuigawa kwao ili waipande.
Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi wa Uzalishaji wa Mazao Wizara ya Kilimo Bi. Beatrice Banzi amesema lengo la kikao hicho inatokana na utafiti uliofanywa na Wizara hiyo siku za nyuma baada ya Mkoa wa Morogoro kuonesha nia ya kulima zao hilo.
Kwa sababu hiyo wizara ilifanya utafiti na kugundua kuwa sehemu kubwa ya Mkoa huo inaweza kustawisha zao la karafuu hivyo kuongeza kipato cha wananchi na kuhifadhi mazingira kwa sababu miti ya mikarafuu hafyuzi maji.
Katika utekelezaji wa azma hiyo, Wizara imetafuta miche 235,000 ya mikarafuu kwa ajili ya kupandwa mkoani humo. Bi. Beatrice amebainisha kuwa kabla ya kupewa miche hiyo baadhi ya wakulima watapelekwa kupata mafunzo ya siku tatu katika kituo cha kuzalisha miche cha Mlingano cha Mkoani Tanga ili kupewa ujuzi wa kustawisha zao hilo na baada ya mafunzo hayo watapewa miche hiyo tayari kwa kupandwa.
Kwa upande wake Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Uchumi na Uzalishaji Mali Dkt. Rozalia Rwegasira amesema yeye pamoja na watendaji wenzake wa Sekta ya Kilimo na Uchumi watahakikisha wanatekeleza maono ya Mkoa huo kustawisha mazao ya viungo ikiwemo zao la karafuu hivyo kujulikana kama Morogoro Spice Aroma Hub lakini pia kurudisha uoto wa asili wa Mlima ya Uluguru.
Naye Afisa Kilimo Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro Chesko Lwaduka amesema katika kuongeza thamani ya mazao ya viungo yakiwemo iliki, mdalasini tangawizi,vanila karafuu na Pilipili manga kwa mwaka 2023 wameweza kusambaza bure kwa wananchi miche 30,000 ya mikarafuu pamoja na kuandaa kitalu kingine cha miche 100,000 kwa ajili ya mwaka ujao.
MWISHO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.