Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Ali Malima amesema Serikali ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imeweka mikakati Mkoa wa Morogoro kuwa Mkoa wa kilimo biashara ambapo Wilaya ya Gairo itakuwa mfano wa kuigwa katika ajenda ya kukuza kilimo.
Mhe. Malima amesema hayo Oktoba 10, 2023 katika ufunguzi wa maonesho ya kilimo biashara na kilimo marathon yanayofanyika Wilayani Gairo yakiwa na lengo la kukuza kipato cha wananchi sambamba na kukuza mapato ya Halmashauri kupitia sekta ya kilimo.
Mhe. Adam Malima amesema mkakati huo utakaoanzia Wilayani Gairo katika kilimo cha mazao ya mahindi na alizeti kuongeza tija ya uzalishaji unalenga kuzalisha kutoka gunia tano za mazao hayo kwa ekari hadi gunia 25.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Ada
"...twendeni tukaigeuze Morogoro kama alivyokusudia Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan Morogoro ikawe ndio Mkoa wa kimkakati katika uzalishaji wa kilimo Tanzania..." amesema Mhe. Adam Malima
Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa amemuagiza Katibu Tawala msaidizi sehemu ya uchumi na uzalishaji Dkt. Rozalia Rwegasira kushirikiana na wadau mbalimbali wa Wilayani humo kutoa elimu ya msingi juu ya kilimo biashara kwa wakulima ili kuwa na uzalishaji wenye tija.
Sambamba na hilo Mhe. Malima amewataka Wakurugenzi, Maafisa ugani, Maafisa tarafa, Maafisa watendaji wa kata na vijiji kufahamu masuala ya msingi ya kilimo na kuhakikisha wanawahimiza wakulima kutumia mbegu, mbolea na mbinu za kisasa kwa uzalishaji wenye tija huku wakitunza mazingira ambayo ndio chanzo kikubwa kwenye kilimo.
Mkuu wa Mkoa amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa dhamira yake ya kutaka Mkoa huo kuwa wa kimkakati kwani amesema sekta ya kilimo Mkoani humo ina thamani zaidi ya shilingi trilioni 2 kukiongozwa na mazao ya mpunga na miwa.
Kwa upande wake, Katibu Tawala msaidizi sehemu ya uchumi na uzalishaji Mkoani Morogoro Dkt. Rozalia Rwegasira amesema maonesho hayo yatawaelimisha wakulima namna ya kutumia mbinu bora za kilimo kuanzia matumizi ya mbegu bora, mbolea, viua wadudu na teknolojia za kisasa huku akiwatahadharisha wakulima juu ya uwepo wa mvua za El-nino ambapo amewataka kuandaa mashamba yao mapema ili kuwa tayari kwa kupanda.
Katika hatua nyingine, Mkuu wa Wilaya ya Gairo Mhe. Jabir Makame akimkaribisha Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima amesema Wilaya hiyo imeanza kutekeleza wa ajenda ya kilimo biashara kwani wakulima zaidi ya 98% hutegemea shughuli za kilimo hata hivyo amesema wakulima hao hawazalishi kwa tija na kwamba maonesho hayo yanaenda kutatua changamoto hizo na kuongeza uzalishaji wenye tija.
Nae, Mbunge wa Jimbo la Gairo Mhe. Ahmed Shabiby ameipongeza serikali ya awamu ya sita kwa kuhakikisha wananchi wa Wilaya hiyo wanapewa umeme na kuomba umeme jazilizi kwa baadhi ya vijiji ambavyo havina umeme kwani amesema nishati hiyo inasaidia wananchi kutekeleza shughuli zao mbalimbali za kiuchumi ikiwemo shughuli ya kilimo.
Mwisho.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.