Mkoa wa Morogoro umejipanga kutoa asilimia 70 ya sukari itakayozalishwa hapa nchini kupitia viwanda vitatu vya sukari vya kilombero, Mtibwa na Mkulazi vilivyopo Mkoani humo.
Mwenyekiti wa Makampuni ya Super Group Bw. Seif A. Seif akimuonesha Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima baadhi ya mitambo ya kiwanda cha sukari cha Mtibwa kinachozalisha sukari hapa nchini.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima akitoa maelekezo kwa uongozi wa kiwanda hicho cha sukari.
Hayo yamebainishwa Septemba 10 mwaka huu na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Malima wakati akizungumza na Viongozi na wafanyakazi wa kiwanda cha sukari cha Mtibwa kilichopo Wilayani Mvomero wakati wa ziara yake ya siku moja kiwandani hapo.
Mhe. Malima amesema kwa sasa mahitaji ya sukari hapa nchini ni zaidi ya tani 600,000, kupitia Viwanda vya kilombero, Mtibwa na Mkulazi vitazalisha zaidi ya tani 400,000 hivyo kufanya Mkoa wa Morogoro kutoa asilimia 70 ya mahitaji hayo ya sukari hapa nchini na hii ni kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Viwanda hivyo na kupelekea nchi kujitegemea kwenye bidhaa hiyo.
"...uzalishaji wetu kwa viwanda vitatu vya Mkoa wa Morogoro tunatarajia kuzalisha tani 400,000 meaning what kwenye uzalishaji wote wa sukari Tanzania nzima asilimia 70 ya mahitaji ya sukari yatakuwa yanatoka Morogoro..." amesema Mhe. Adam Kighoma Malima.
Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa ameipongeza Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuweka Sera nzuri na mazingira wezeshi ya uwekezaji ambayo yamewafanya wawekezaji kujiamini kuwekeza hapa nchini.
Sambamba na hilo, amekipongeza kiwanda cha Mtibwa kwa kuweka mikakati ya kuongeza uzalishaji wa sukari na zao la miwa, hivyo ameutaka uongozi wa kiwanda hicho kutoa elimu kwa wakulima ili waongeze uzalishaji wa miwa ambapo kwa sasa wakulima hao wanachangia asilimia 10 ya miwa kiwandani hapo.
Katika hatua nyingine, Mhe. Malima ameutaka uongozi wa Mtibwa kutoa elimu kwa wafugaji kufuga kibiashara hususan katika kunenepeshaa ng'ombe wao ili kuwasaidia wafugaji Mkoani humo kuacha kufuga kimazoea.
Naye, Mwenyekiti wa Makampuni ya Super Group Bw. Seif A. Seif amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa Sera nzuri za uwekezaji ambazo zimewafanya kuendelea kuwekeza katika nyanja mbalimbali za kijamii, kilimo, ufugaji na uvuvi.
Kwa upande wake Meneja wa Shamba la miwa la Dakawa 1 Bw. Selemani Juma amesema uzalishaji katika shamba hilo unaongezeka kila mwaka kutokana na uwekezaji uliofanywa na kiwanda hicho kwa kusaidiwa na Serikali kusimamia sera ya uwekezaji.
Meneja wa shamba la miwa la Dakawa 1 Bw. Selemani Juma akiwasilisha taarifa ya shamba hilo kwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro (hayupo pichani)
Aidha, amesema kiwanda hicho kimeweka mikakati ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi kwa kuweka mifumo mbalimbali ya kisasa ya uvunaji wa maji na umwagiliaji ili kuongeza uzalishaji wa zao la hilo miwa.
MWISHO.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro
Sanduku la Posta: S.L.P 650 MOROGORO
Simu: +2550232934305
Simu: +255766828252
Barua pepe: ras.morogoro@tamisemi.go.tz
Haki Miliki © 2024 Ofisi Ya Mkuu wa Mkoa Morogoro. Haki Zote Zimehifadhiwa.